Mahakama ya Hakimu Makazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo imemwachia huru mfanyabiashara James Rugemalira baada ya kukaa mahabusu kwa muda wa miaka minne (2017-2021).
Rugemalira alifahamika zaidi katika kipindi cha kesi hiyo iliyovutia Wafuatiliaji kutoka kote duniani ambapo alikuwa Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa kampuni ya IPTL kwenye sakata hilo la Tegeta Escrow.
Machache ya kufahamu kuhusu yeye ni kwamba alikuwa mwajiriwa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) lakini aliacha kazi mapema na kuingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisoma Shahada ya awali ya Biashara (B.Com).
Akiwa mkurugenzi VIPEM Ltd alikuwa kiungo muhimu kwenye kufanikisha dili la IPTL. Jukumu kubwa alilokuwa nalo wakati huo lilikuwa kuisaidia IPTL kuvuka urasimu nchini, ambapo mradi huo ulizinduliwa miaka saba tangu kusainiwa kwa makubaliano (MOU).
Washirika wake katika biashara (Tritel, IPTL) na mawakala wa usambazaji (Windhoek, Heineken) walijikuta mahakamani kwa mashitaka mbalimbali. Inadaiwa kuwa Rugemalira alitumia kesi hizo kujitajirisha, na kuwa miongoni mwa watu wenye ukwasi nchini, huku yeye akishtakiwa kwenye mahakama za kimataifa.
Kesi ya mwaka 2001 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID) ilitokana na mkakati wa IPTL kupandisha gharama za mkataba (EPC).
Katika moja ya mahojiano yake kuhusu dili la IPTL, Rugemalira alisema kuwa Watanzania wenzake wanatakiwa wamchukulie yeye kama shujaa na mzalendo kwa sababu dili hilo lilifanyika kwa maslahi ya Taifa. “Nilistahili $ 600 milioni, lakini nilichukua $75 milioni, ambayo ni kidogo…”
Washitakiwa wengine waliokuwa naye kwenye kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni Harbinder Sethi na Joseph Makandege.