Mako, mpwa wa Mfalme wa Japani Nahurito, amezama kwenye penzi zito la kijana Komuro ambaye ni Mwanasheria. Ndoa ya Mako na Komuro inatarajiwa kufungwa tarehe 26 Oktoba 2021, na uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa na Idara ya Habari ya ngome ya Mfalme nchini Japan.
Mako na Komuro walikutana wakiwa wanafunzi wa ‘Tokyo International Christian University’. Mako mwenye umri wa miaka 29 alivishwa Pete na Komuro mnamo 2017 na kutangaza kufunga ndoa mapema 2018.
Lakini mipango ya ndoa yao iliingia dosari baada ya Mama yake Mzazi Komuro na mpenzi wake wa zamani kuingia katika mgogoro wa kifedha uliomuhusisha Komuro ambapo mgogoro ulizua skendo kubwa hadi ndoa hiyo kughairishwa.
> Vanessa Mdee ashambuliwa kisa wigi alilovaa
Agosti 2018 Komuro aliondoka nchini Japan, kwenda Marekani kuendelea na masomo ambapo hakurudi tena hadi Jumatatu ya wiki iliyopita.
Utata na mgogoro uko katika ukweli kwamba, ndoa ya Mako na Komuro inavunja mila na desturi za ngome ya kifalme ya Japan, na endapo Mako ataolewa kweli na kijana Komuro, basi harusi yao itafanywa kama ya watu wa kawaida tu, huku Mako akivuliwa nyadhifa zote za ufalme na kubaki kama raia wa kawaida.
Kulingana na mila za ngome ya kifalme ya Japan endapo Mako asingekubali kuolewa na Komuro na akakubali kuolewa na mchumba ambaye ngome ya Japan imemridhia, basi Mako angefanyiwa harusi ya gharama inayofikia shilingi bilioni Mbili za kitanzania.
Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida Mako amekataa kabisa harusi hiyo na anakuwa binti wa kwanza kutoka ngome ya kifalme kufanya hivyo.
Baada ya ndoa yao Mako na Komuro wataenda nchini Marekani na kuishi maisha ya kawaida ambapo Komuro amepata ajira katika kampuni ya sheria nchini humo.
Tukio hilo limeibua hisia kali sana nchini Japan, huku wengine wakimsifu Mako kwa uamuzi wake, na wengine wakipinga uamuzi huo na kusimama pamoja na ngome ya kifalme.