Kauli ya Rais Samia kuhusu tozo

HomeKitaifa

Kauli ya Rais Samia kuhusu tozo

Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kupunguzwa kwa tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta  hapa nchini zenye thamani ya shilingi bilioni 102 kwa mwaka, kwa lengo la kupunguza bei za mafuta ili kuwapa unafuu wananchi.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Oktoba 5, 2021 wakati akipokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Nishati, January Makamba kuhusu utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa wizara hiyo kupitia mwenendo wa biashara ya mafuta na bei zake hapa nchini.

Utekelezaji wa maagizo hayo umeenda sambamba na marekebisho ya Kanuni mbalimbali zinazohusiana na tozo na yatachapishwa katika Gazeti la Serikali leo tarehe 05 Oktoba, 2021.

Rais Samia amechukua hatua hii ili kukabiliana na upandaji wa bei za mafuta katika soko la dunia ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikipanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri watumiaji wa bidhaa hiyo hapa nchini.

   > Boss Shell, apongeza maboresho mazingira ya uwekezaji Tanzania

Taasisi zinazoguswa na maelekezo ya kupunguzwa kwa tozo hizo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (tozo ya udhibiti), Mamlaka ya Bandari (tozo ya miundombinu), Mamala ya Mapato Tanzania ( tozo ya kuchakata taarifa), Shirika la Viwango Tanzania ( tozo ya kupima ubora wa mafuta kwenye meli na gharama ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta), Wakala wa Vipimo Tanzania (tozo ya uhakiki wa ujazo wa mafuta melini), Wakala wa Usimamizi wa Meli (tozo ya forodha) na Mamlaka ya Serikali  za Mitaa (ushuru wa huduma kwenye Halmashauri nne zenye maghala ya kupokea mafuta kwa jumla).  Halmashauri hizo ni Kigamboni na Temeke za Jijini Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Aidha, Rais Samia ameagiza ufanyike mchakato wa haraka wa kupeleka marekebisho ya Sheria Bungeni endapo zipo Sheria nyingine zinazohitaji marekebisho ya haraka katika kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta hapa nchini, ili kumlinda mtanzania na gharama za maisha zinazotokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

error: Content is protected !!