Rais akoshwa majengo ya mahakama kutenga maeneo kwa wanaonyonyesha

HomeKitaifa

Rais akoshwa majengo ya mahakama kutenga maeneo kwa wanaonyonyesha

Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kufurahishwa na majengo ya mahakama yaliyojengwa katika mikoa mitano nchini kutenga maeneo kwa makundi maalum ikiwemo wanawake wanaonyonyeshe.

Rais Samia amesema hayo wakati wa uzinduzi vituo jumuishi vya utoaji haki ambavyo vipo sita nchi nzima katika mikoa mitano ya Arusha, Mwanza, Morogoro, Dar es Salaam (2) na Dodoma ambacho amekizindua leo kwa niaba ya vituo vingine vitano.

Amesema kuwa ujenzi wa jengo majengo hayo yanaendana na karne 21, pia yamezingatia makundi ya wanawake pamoja na watoto, akitolea mfano majengo yaliyokuwepo ambayo endapo mama akitaka kunyonyesha mtoto, ilimlazimu kutafuta uchochoro wa kujificha, akimaliza ndio arudi mahakamani.

“Jengo ni zuri na linaendana na karne ya 21. Nimeliangalia wakati napata maelezo nikaambiwa bilioni 9 nikanyanyua uso kuangalia zimeingia wapi lakini nilivyoingia ndani nimeona vilivyokaa kwa hiyo kwa jengo hili thamani ipo sawa sawa.”

Pamoja na hayo, wakati wa hotuba yake Rais ameelezea changamoto zilipo kwenye mahakama ikiwemo watu kucheleweshewa haki, hivyo amewasihi wahusika kuongeza kasi katika kutoa haki na kutaka jicho la ziada kumulika mahakama za mwanzo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa sana katika suala la utoaji haki.

Raisi Samia amesema serikali itaendelea na maboresho ya mahakama katika nyanja za majengo, teknolojia na watumishi kwani watendaji wa mahakama wanatakiwa kufanya
kazi katika miundombinu mizuri tofauti na ilivyokuwa zamani.

Kwenye kutambua umuhimu wa shughuli za mahakama, amesema mahakama ni chombo cha mwisho kutoa haki, kinawezesha kukuza uchumi na muhimili wa kudumisha amani kwani wanasuluhisha migogoro inayotokea kwenye jamii.

Amewashukuru watumishi wote wa mahakama na kuahidi serikali itaendelea kuboresha mahakama, kuongeza watumishi na kuangalia maslahi ya watendaji.

error: Content is protected !!