Mgogoro wa China – Taiwan wafikia pabaya

HomeKimataifa

Mgogoro wa China – Taiwan wafikia pabaya

Waziri wa Ulinzi wa Taiwan Chiu Kuo-Cheng amesema kuwa hivi sasa mgogoro wa China na Taiwan umefikia hatua mbaya zaidi kuliko wakati wowote katika kipindi hicho ndani ya miaka 40 iliyopita.

Waziri huyo wa Ulinzi ameonya kuwa China inaweza kuivamia nchi hiyo moja kwa moja ifikapo mwaka 2025. Tamko hilo limetoka Serikali ya Taiwan baada ya Taifa la China kurusha ndege zake za kivita kwenye anga ya Taiwan ndani ya siku nne mfululizo.

Wakati Waziri huyo akiongea mbele ya kamati ya Bunge, alihimiza Bunge la nchi hiyo kupitisha muswada ambao utaweza kuifanya Serikali kutumia fedha nyingi hasa katika ulinzi, kununua makombora ya masafa marefu na meli kubwa za kivita.

China na Taiwan wana Mgogoro gani?

Taiwan inajiona ni nchini kamili na huru, lakini China inaiona Taiwan sio nchi bali ni sehemu halali ya China iliyojitenga hivyo China inakusudia kuchukua eneo lako siku moja.

Ipo sera inayoitwa ‘Sera ya China moja’ (One China Policy), ambayo inaeleza China ni moja tu, hivyo basi kwa taifa lolote duniani kama linataka kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na China, basi ni lazima lisiwe na uhusiano wa kidiplomasia na Taiwan. Sera hii ni uti wa mgongo kwa China kwenye kuunda sera zake za mambo nje.

Hata Taifa la Marekani mnamo mwaka 1979, lilifunga ubalozi wake nchini Taiwani na kufungua ubalozi wake China kutokana na ushawishi na umuhimu wa Taifa la China. Licha ya Marekani kufunga ubalozi wake Taiwan, lakini iko sheria maalum ya Marekani ambayo inaifanya Marekani na Taiwan kufanya biashara hasa katika kuiuzia silaha za kivita ili iweze kujilinda.

Chanzo cha mgogoro ni nini?

Chanzo cha mgogoro huu ni baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe kuisha mwaka 1949. Walioshindwa vita walikimbilia Taiwan na Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) waliunda Serikali ya Jamhuri ya China Beijing. Pande zote mbili, Taiwan na China, walianza kujinadi kuwa wao ndio China halisi.

Tangu wakati huo, China na Beijing imekuwa ikiitishia Taiwan kuwa itaivamia kijeshi kama Taiwan itatangaza uhuru wake, na China imekuwa ikisisitiza iko siku Taiwan itakuwa sehemu ya China, hata kwa kutumia nguvu ikibidi.

error: Content is protected !!