Kama unapitia changamoto kuhusu jinsi gani utakuza uchumi wako ikiwa hauna mtaji wa kuanzisha biashara au haujui wapi utaajiriwa, basi ujuzi wako unaweza kukusaidia kupata kazi kwenye tovuti mbalimbali. Hii hapa ni orodha ya tovuti unazoweza kufanya kazi ukiwa nyumbani na ukajipatia kipato.
1. 99 Designs
Hii ni tovuti inayowakutanisha watu wanaomiliki makampuni au biashara mbalimbali pamoja na watu wenye taaluma ya kubuni michoro na picha kwa ajili ya kutumika kama vielelezo vya bidhaa za kampuni husika. Wamiliki wa biashara huandaa shindano na kuweka vigezo vyao, unachotakiwa kufanya ni kujiunga na kushiriki shindano litakalokuwepo na ikitokea umeshinda unapata fursa ya kutengeneza na kupata pesa.
2. Upwork
Hii ni tovuti ambayo ina waajiri zaidi ya watu milioni 1.5 ambao wanatafuta wafanyakazi. Tovuti hii inatoa ajira za muda mfupi na muda mrefu kulingana na taaluma uliyonayo mfano kuna nafasi za watu wa mauzo na masoko, teknolojia ya habari, wahasibu n.k.
3. Fiverr
Kwenye tovuti hii mfanyakazi ndiye anaweka kazi zake kwenye tovuti na kuziuza kuanzia Dola 5 (Tshs 11,525) kwa mfumo wa kazi za muda mfupi, hivyo mwajiri humfikia mfanyakazi kwa kutafuta jambo linaloendana na kazi zake.
> Ajira rasmi 10 zinazolipa zaidi nchini Tanzania
4. College recruiter
Wanafunzi ambao wamemaliza chuo muda mfupi wanaweza kutumia tovuti hii kupata kazi za muda mfupi. Ni sehemu itakayosaidia kujenga uwezo wa kile mtu alichokisomea kabla ya kupata ajira ya moja kwa moja.
5. Toptal
Hapa inabidi mtu afanye usaili kwanza ili waweze kujua uwezo wake na endapo atafanikiwa usaili atapata nafasi ya kufanya kazi na kampuni kubwa ambazo hutafuta wafanyakazi wa muda mfano wa kampuni hizo ni Airbnb, Zen desk na JP Morgan.
6. Peopleperhour
Tovuti hii ni mahsusi kwa wasanifu wa kimtandao yaani watu wanaoweza kutengeneza tovuti, kutengeneza video, watafsiri, waandishi n.k unaweza kujisajili na kuweza kupata kazi ya muda itakayokulipa.