Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi, yuko Tanzania kwa ziara kikazi ambapo leo akiongozwa na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan wamezungumza na waandishi wa habari.
Katika hotuba zao, Rais Samia na mgeni wake Rais m Ndayishimiye wamezungumza mambo mengi ikiwa ni maeneo ya ushirikiano baina ya nchi zao.
Tumekukusanyia mambo sita ambayo yaliyatajwa katika hotuba za Marais hao:
6. Ushirikiano wa kindugu
Rais Evariste Ndayishimiye amesema kwamba kwao wao (Warundi), Watanzania sio rafiki zao bali ni ndugu zao. Akaeleza kwamba undugu huo ulikuwepo kwa miaka mingi tangu enzi za Mwalimu Nyerere, na kwamba Tanzania imekuwa ikiwapa hifadhi raia wengi wa Burundi waliokuwa wakikimbia vita nchini mwao.
Naye Rais Samia Suluhu amesema Tanzania inaridhishwa na uhusiano mzuri wa kindugu baina yake na Burundi.
5. Ulinzi
“Tanzania inaichukulia Burundi kuwa ni ndugu, rafiki na mshirika wa karibu katika kuhakikisha kwamba eneo la Maziwa Makuu linakuwa salama lenye amani na utulivu,” ni maneno ya Rais Samia Suluhu alipozungumza kuhusu ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Burundi katika ulinzi na usalama.
Kwa upande wake Rais Ndayishimiye, amesema licha ya jitihada kubwa katika kuimarisha ulinzi, ipo hofu ya kiusalama inayoletwa na kundi linaloongozwa na mwanasiasa wa Burundi, Alexis Sinduhije akishirikiana na kundi la ADF. Hivyo ameomba ushirikiano zaidi katika kulinda amani.
4. Madini
Rais wa Burundi, Evariste Ndeyishimiye amesema nchi yake haijapiga hatua kubwa katika sekta ya madini, hivyo inatarajia kujifunza utaalamu kutoka Tanzania ambapo hati ya makubaliano ya kushirikiana katika sekta hiyo tayari imesainiwa.
Rais Samia naye amegusia eneo hilo la madini kwa kusema “Tanzania tumeshatoa leseni kwa ile kampuni ya Kabanga Nickel. Kampuni ile mbali na kuchimba ‘nickel’ watajenga kiwanda cha kuchakata madini hayo na hivyo hilo ni soko kwa serikali ya Burundi kuuza ‘nickel’ yake hapa [Tanzania].”
3. Ujenzi wa Reli
Rais Samia amesema makubaliano ya kuunganisha mtandao wa reli kati ya Tanzania na Burundi, yatatekelezwa kama ilivyoafikiwa mwezi Januari mwaka huu. Maneno ya Rais Samia yalitiliwa mkazo na Rais Ndeyishimiye aliyesema kwamba nchi hizo mbili (Tanzania na Burundi) tayari zimekubaliana kuhusu njia za kufadhili ujenzi wa reli kutoka Uvinza Kigoma hadi Musongati Burundi.
Rais Samia ameeleza kwamba katika ujenzi wa reli hiyo, kilomita 160 zitakuwa upande wa Tanzania, na kilomita 180 zitakuwa Burundi.
2. Kilimo
“Kampuni ya Burundi ya Itracom inayotengeneza mbolea tayari imewasili Tanzania na itaajiri wafanyakazi wa Burundi na Tanzania kwa usawa. Tanzania itanufaika sana, na suala la uagizaji mbolea litatoweka, na fedha zitawekezwa kwenye sekta nyingine,” ni maneno ya Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi akiongelea ujenzi wa kiwanda cha mbolea ikiwa kati ya maeneo muhimu yatakayoinufaisha sekta ya kilimo kupitia ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi.
Aidha, Rais Ndeyishimiye ameeleza kwamba Burundi imeiomba Tanzania kuipatia maeneo kwa ajili ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kilimo cha miwa ili kuweza kuongeza uzalishaji wa sukari nchini Burundi.
1. Bandari
“Kulikuwa na ombi la Burundi kupatiwa eneo la ujenzi wa bandari kavu pale Kwala Ruvu mkoa wa Pwani na Katosho, Kigoma. Tanzania tulishawasilisha rasimu ya mkataba upande wa Burundi nasi tunasubiri maoni yao ili kazi iendelee,” ni maneno ya Rais Samia Suluhu wa Tanzania, ambayo yaliakisiwa katika hotuba ya Rais Ndayishimiwe aliyesema ujenzi wa bandari kavu katika maeneo hayo utapunguza gharama za usafirishaji.
Mambo mengine yaliyozungumzwa na Marais hao ni pamoja mapambano dhidi ya UVIKO-19 na ushirikiano wa kikanda ambapo Burundi imeipongeza Tanzania kwa jitihada zake katika kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.