Ijue Historia ya watu wa Tanga kuitwa wavivu

HomeMakala

Ijue Historia ya watu wa Tanga kuitwa wavivu

Mji wa Tanga ni moja ya miji mkongwe sana hapa nchini, ni moja kati ya sehemu zilizoanza kupata ustaarabu wa jamii nyingine kama wahajemi, wareno na waarabu mapema sana kabla ya sehemu nyingine Tanzania. Katika Dini, Uchumi, Siasa, Mazingira, Sayansi na vitu vingine, mji wa Tanga uliwahi kuwa kati ya miji ya awali kabisa katika pwani ya Afrika Mashariki kupata vitu hivyo. Ndani ya mji wa Tanga athari za wageni bado zimo nyingi tu, katika vyakula walavyo, nguo wavaazo, dini waabudizo, lugha wazungumzazo na mengineyo katika maisha yao ya kila siku. Kwani walikaa wageni kwa jumla miaka zaidi ya 800.

Wakati wa utawala wa wajerumani, haina maana kuwa waingereza hawakuwepo, walikuwepo ila kama wamisionari na sio watawala, waingereza walichukua koloni baada ya vita ya kwanza ya Dunia (1914 – 18). Wamisionari ni watu walioeneza dini ya kikiristo, hata kanisa la kwanza kujengwa nchini, lilijengwa Tanga eneo la Magila Muheza 1843, lilikuwa ni Anglican ambalo kwa asili ni la uingereza, halafu 1847 wakafuata nao kujenga kanisa Lutheran huko huko Tanga, ambao kwa asili nao ni Ujerumani.

Sasa, huu wakati wa kueneza dini, elimu ya kimtaala (formal education) na harakati za kilimo cha mkoloni (Commercial Agriculture), ndio dhana ya ‘UVIVU’, na watu wa Tanga iliposhika kasi, na tukisema watu wa Tanga ni wavivu, kuna tofauti kati ya dhana hiyo ikitamkwa ndani ya Tanga na nje ya Tanga, ndani ya Tanga, makabila mengine husema kuwa, kabila la ‘Wadigo’ ndio wavivu, ila ukienda mikoa mengine, unasikia kwa ujumla wake, yaani watu wote wa Tanga ni wavivu; wadigo, wasambaa, wabondei, wazigua, wanguu, na makabila mingine, je hii ni kweli na ni kwa nini?

Kama nilivyobainisha hapo awali, elimu ya kimtaala, Dini na vitu vingine kama kilimo cha kisasa, Tanga ilipata bahati kuvipata mapema, na ndio kilikuwa kipindi hicho dhana ya watu wa Tanga kuwa ni ‘WAVIVU’ iliwaganda hadi leo hii. Wakati waingereza (Missionaries) wanafika Tanga, tayari wadigo walishafika kutoka Shungwaya au kashuri Somalia, eneo ambalo kwa sasa linaitwa Mogadishu, mwanzoni mwa karne ya 12 hadi 14 walikuwa wanahama taratibu, kitabu cha ‘Mijikenda Agriculture in the Coastal Province of Kenya’ kilichoandikwa na ‘Henk Waaijenberg’ kinaeleza kisa cha wadigo vizuri tu kutoka huko walipotoka mpaka kuwapo Kenya na Tanzania leo hii.

Wadigo hawa na watu wengine waliowakuta pwani, walikuwa 100% ni waislamu, ukiachilia mila na dini yao zingine za asili. Wakati Ukiristo unaanza, Tayari uisilamu ulishakita mizizi pwani miaka ziaidi ya 400 nyuma, hivyo mkakati wa kuwabadili hawa watu kutoka kwenye dini moja kwenda nyingine, ulikuwa mkakati mgumu sana, kuna watu walikufa, wengine walitengwa, wengine wakahama na kadhia za kila namna.

Sasa, katika makabila yote haya waingereza waliyoyakuta Tanga, Wadigo ndio watu ambao walikuwa wagumu, wenye tabu, vita na matatizo makubwa sana kwenye kupokea Ukiristo na Elimu ya kumtaala, ila jamii kama za wasambaa na wabondei, hawa ilikuwa rahisi tu na ndio maana hata maendeleo ya elimu na kilimo kwao vilionesha matunda mapema sana, kuliko kwa wadigo, kwa wale watu wa Tanga mtakubaliana na mimi, hadi leo kuna tofuati tunaziona kwa jamii hizi, shule za kwanza, makanisa, zahanati, zilijengwa wa kwa jamii za wasambaa na wabondei, haina maana kuwa kwa wadigo wakujenga, waingereza walijenga shule moja huko Manyinyi ngombero, mwalimu akiwa mzee Paul Pera, kati ya wadigo wa awali kukubali Ukiristo, shule ile wadigo walichoma moto ikawa jivu kabisa, wadigo hawakutaka kabisa kusikia kitu Ukiristo, kwani dini na elimu kipindi hicho vilienda pamoja.

Licha wadigo kugoma kabisa, ila mchungaji wa kwanza kabisa wa Lutheran Tanzania, alikuwa mdigo mwenye asili ya Mombasa, wazazi wake wake walihama na walimzaa Tanga (1888), aliitwa Jacob Lumwe au Jacob Ng’ombe. Mambo ambayo wadigo waliyakataa kabisa, ilikuwa rahisi kwa jamii nyingine kuyakubali, hivyo ikawa muingereza amefanikiwa kuwagawa, mjajua wenyewe elimu inavyogawa watu watu na kulete matabaka katika jamii, baada ya muda wadigo wakawa wako chini, makabila mengine yako juu. Wakaanza kucheka waafrika, walisahau kuwa adui yao ni aliyewatenganisha, licha hata hao wenyewe walishawahi kuwa na tofauti baina yao kabla ya kuja kwa mzungu. Wadigo wengi waliosoma na huko ndio utakuta pia kuna wakiristo wengi, ni wadigo wa ‘Gombero’.

Ila kote kote kulikobaki, utakuta 100% waisilamu. Katika jamii ya wabondei, ni kawaida kukuta familia moja au uko kuna mchanganyiko wa waislamu na wakiristo, hata wasambaa, maana wengi walilazmika wabadili dini wakasome, ndio utakuta mtu anaitwa ‘George Ramadhan’. Tanga, ukitazama elimu ya Dini ya Kiislamu ipo kwa Wadigo, hata mashekhe wakubwa wa kwanza kwanza na madrasa zilizowahi kutamba na bado zinafanya vyema, utakuwa watu wenye jamii ya udigo, ndio wazuri sana, ukiristo sio sana, maana hii tangu a tangu wilichagua kushika utamaduni ni dini walioleta waarabu. Na upande wa pili, ukitaka ukiristo, nenda kwa wasambaa na wabondei, na hao ndio wana elimu ya kimtaala waliipata vyema pia.

Wadigo waliitwa wavivu, kukataa elimu, waingereza walitumia njia hii kusambaza propaganda mbaya juu ya wadigo, jamii nyingine waliwacheka sana kuwa wao sio wasomi, na kila walipoenda waliwasema hivyo sifa hiyo ikawaganda na muingereza kiulaini kabisa akafanikisha malengo yake. Licha tu ya kugomeo elimu, wadigo huko kenya maeneo ya kilifi na Tanzania Kwale, waligomea hadi kilimo, hapo awali walikuwa wakilima kwa juhudi sana mazao kama mahindi, maharage, mihogo, minazi na mazao mengineyo – ila, waingereza waliwataka wapunguze mazao ya chakula na walime mazao ya Biashara kama Kahawa, Korosho, michikichi, Pamba na mengineyo, mazao haya wadigo waliona hayana faida kwao bali kwa waingereza, waligoma pia na wengine wakakubali, hapa sasa ndio rasmi wakawachachika jina la ‘BACKWARD SOCIETY’ (Jamii ya watu waliopitwa na wakati). Hiki kiilikuwa kicheko kwa makabila mengine dhidi ya wadigo.

Ukiachilia mbali hayo yote, Tanga kuanzia mwaka 1920, baada ya Muingereza rasmi kuchukua koloni,. Mashamba ya Mkonge yaliyokuwa chini ya mjerumuma, serikali ya Uingereza iliamua kuyabinafsisha kwa makampuni binafsi. Makampuni yale yaliunda umoja wao na kuuita TSGA (Tanganyika Sisal Growers Association), ambapo ofisi zao ndio pale ‘Mkonge Hotel kwa sasa. Makampuni yale yalianza kutumia wakazi wa Tanga kulima mkonge, kulingana na mazingira magumu ya kazi, watu walianza kukimbia, watu walikimbia sana hadi mashamba yakakosa wafanyakazi.

Mkurugenzi Mtendajii wa TSGA raia wa Uingereza na Mwenyekiti wa Kampuni ya Bird & Company aliyeitwa Sir Harry William Lead, aliweza kutumia ushawishi wake kwenye baraza la TSGA na kuandaa muswada utakaowezesha kuanza kuchukua ‘manamba’ au wafanyakazi wa mashamba ya mkonge kutoka mikoa ya bara hadi Rwanda na Burundi. Ukisoma kitabu cha M.G Tenga ‘Sisal Industry in Tanzania since Colonial Era’ utaona habari zote hizi.

Sheria ilipitishwa mwaka 1923 iliitwa ‘Labor and Native Ordinance Act’, iliwaruhusu watu waingereza kaichukua manamba kutoka Mbeya, Singida, Dodoma, Songea na mikoa mingine hadi Rwanda na Burundi, watu hawa ilikuwa ngumu sana wao kukimbia kwakuwa walikuwa wageni Tanga. Ila wakati wanafuatwa waliahidiwa vitu vizuri kama Pesa, Baiskeli, Makazi bora na hawakuambiwa kuwa wanakwenda kulima mkonge, walikubali na hatimaye hawakukuta hata kimoja, walifanya kazi katika mazingira magum mno, walipoteza maisha kwa maradhi kama malaria, Kifua kikuu, typhoid na ajali kazini pia ziligharimu sana maisha yao.

Ila kwakuwa watu wa Tanga tayari walishakimbia mashamba wakabaki wachache tu, tayari maeneo mbali mbali wanajua watu wa Tanga ni wavivu hawataki kazi na hadi leo jina hilo limewaganda. Wadigo na watu wa Tanga sio wavivu katu, na ni vibaya sana kuwaita hivyo, kwani kazi zinafanyika ma matokeo yanaonekana.

kila sehemu duniani kuna watu wavivu, uvivu sio wa jamii fulani tu au watu fulani. Kuita watu fulani wavivu au kabila fulani hasa watu wa Tanga ambao kimtazamo wangu ndio wa hanga wa neno hili, ni kudumisha propaganda ya wakoloni kutugawa na kujishusha thamani wenyewe kwa wenyewe.

Uvivu ni lazima ukemewe, sio kitu chema hata dini zimekemea uvivu. Ila, tuwe tunasoma, tunafuatilia na kung’amua kiundani vyanzo vya vitu duniani sio kusikia tu maneno tukadakia na kusambaza.

error: Content is protected !!