Ukweli ni kwamba wanawake hawapati dalili za kufanana, kila mwanamke yuko tofauti. Vivyo hivyo ndivyo zilivyo dalili zake za ujauzito. Pia ikumbukwe kwamba hata kwa mwanamke huyo huyo aliyewahi kuwa mjamzito, dalili za kila ujauzito zinaweza zisifanane.
Tahadhari nyingine muhimu ni kuwa inawezekana kabisa dalili za awali za ujauzito zikashabihiana na dalili za kuingia na ukiwa kwenye hedhi, hivyo unaweza usitambue kwa urahisi kwamba umepata ujauzito.
- Kukosa kuona siku zako (hedhi)
Kutokuona hedhi nayo ni dalili ya awali iliyozoeleka ya ujauzito. Tafiti zinaonesha kuwa hii moja ya sababu kuu ya kwafanya wengi kukimbilia kupima ili kujua kama kweli ni wajwazito. Hata hivyo, fahamu kwamba kutokuona siku (hedhi) au hedhi kuchelelwa siyo lazima itokane na kuwa una ujauzito.Pia zipo sababu zingine tofauti na ujauzito zinazoweza kuchangia wewe kutokuona hedhi. Baadhi ya sababu hizi ni kuwa na ongezeko kubwa la uzito wa mwili, mabadiliko ya vichocheo (hormone), uchovu kupindukia, msongo, n.k. Baadhi ya wanawake huwa wanakosa hedhi zao baada ya kusitisha matumizi ya dawa za uzazi wa mpango. Kama umechelewa kuona siku na unahisi ni mjamzito pima ujauzito kuwa na hakika. - Uchovu
Uchovu wa kupindukia katika kipindi cha ujauzito ni jambo la kawaida na ambalo huwa linaanza mapema tu katika wiki za awali za ujauzito.Kwa nini unachoka? Hii hutokana na kiwango kikubwa cha kichocheo cha progesterone. Ifahamike kuwa uchovu pia unaweza kusababishwa na sababu zingine kama vile kushuka kwa shinikizo la damu, kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu au pia ongezeko kwenye uzalishaji wa damu. - Maumivu ya tumbo la uzazi pamoja na kutokwa na matone ya damu ukeni.
Baada ya upevushaji wa yai, yai lililorutubishwa hujipandikiza kwenye mji wa mimba. Hii inaweza kusababisha dalili za awali za ujauzito ambazo ni kama kutokwa na matone ya damu na wakati mwingine maumivu ya tumbo la chini ya kitovu.
Matone hutokana na kujipandikiza kwa yai lililorutubishwa kwenye mji wa mimba. Hutokea wakati wowote ndani ya ya siku 12 baada ya yai kurutubishwa.Maumivu ya tumbo la uzazi (chini ya kitovu), huwa yanashabihiana na maumivu ya hedhi, hivyo baadhi ya wanawake huyachukulia kama maumivu ya hedhi.> Faida 5 za kujamiiana kwa mjamzito
Pamoja na kutokwa damu ukeni unaweza kuona ute mweupe mwepesi kama maziwa kutoka ukeni. Ute huu huwa hauna madhara wala harufu na hauambatani na kuwasha. Pale unapokuwa na wasiwasi kuhusu ute huu unaweza kumwona daktari naye atakufanyia vipimo kuona kama una fangasi, bakteria au kalamidia.
- Mabadiliko katika matiti
Mababdiliko katika matiti ni dalili nyingine ya awali ya ujauzito. Kiwango cha vichocheo (hormone) huwa kinapanda kwa kasi baada ya upevushaji. Mabadiliko hayo yanaweza kufanya matiti kujaa, kuwa kama na vitu vinavyochoma choma au hata kuwa na vidonda wiki moja au mbili baada ya urutubishwaji. Unaweza kuhisi uzito kwenye matiti au matiti kuuma yanaposhikwa. Sehemu nyeusi ya chuchu huwa nyeusi zaidi.Kuna sababu zingine zinazoweza kusababisha mabadiliko katika matiti. Ikiwa mabadiliko haya yanatokana na ujauzito basi kuwa na hakika kwamba itachukuwa muda kwa vichocheo kuzoeleka na vitakapozoeleka maumivu nayo huwa yanapungua. - Kichefuchefu
Hii ni dalili maarufu na iliyozoeleka ya ujauzito, hata hivyo si kweli kwamba kila mjamzito hupata kichefuchefu.Sababu halisi ya kichefuchefu haijulikani ingawaje kupanda kwa vichocheo katika kipindi hiki cha ujauzito kunaweza kuwa moja ya sababu. Kichefuchefu katika kipindi cha ujauzito kinweza kutokea wakati wowote ule ila mara nyingi hutokea wakati wa asubuhi.
Katika kipindi hiki kumbuka kula lishe yenye uwiano mzuri ili wewe na mwanao muweze kupata virutubisho vinavyotakiwa. Unaweza kuwasiliana na daktari kwa ushauri zaidi kuhusu chakula unachohitajika kula.
Mwanamke anapokuwa mjamzito anaweza asiwe na dalili hata moja ya zilizotajwa hapo juu. Vilevile anaweza akawa na dalili zote hizo kwa pamoja. Ikiwa dalili mojawapo au zote zinakuletea maudhi basi muone na daktari kwa maelezo zaidi.