Fahamu ulaji unaoweza kukusababishia upara

HomeElimu

Fahamu ulaji unaoweza kukusababishia upara

Sio jambo la ajabu kwa mwanadamu kupoteza nywele, kwa kawaida nywele 50 hadi 100 huweza kung’oka kichwani mwa mtu kwa siku bila mtu kujua.

Taasisi ya Afya nchini Uingereza (NHS) inaeleza kwamba mtu anapopoteza nywele nyingi (zaidi ya 100 kwa siku) anaweza kuwa na upara baada ya muda, jambo ambalo linaweza kusababishwa na mfumo wa ulaji.

Kwa kukosa vyakula vya aina fulani, nywele zinaweza kupungua taratibu, lakini pia zinaweza kupungua kwa kuzidisha aina fulani ya vyakula.

Ulaji wa kwanza unaoweza kusababisha upara, ni ulaji hafifu wa protini. Mwili wako unapokosa protini ya kutosha, unaweza kupoteza kiasi kikubwa cha nywele zako.

Jitahidi kula maharage, karanga, samaki na vyakula vingine vya protini ili ulinde nywele zako.

Jambo lingine linalowezesha kusababisha upara ni ulaji wa Vitamini A kupita kiasi. Pamoja na umuhimu wa Vitamini hiyo inayopatikana kwenye vyakula kama mayai, maboga na mboga nyingi za majani, inapaswa kuwa katika kiwango cha kawaida.

Pia, vyakula hivyo vyenye Vitamin A, vinaweza kuufanya mwili uwe na kiasi kikubwa sana cha madini ya ‘Calcium’ ambayo yanaweza kuathiri nywele na kucha pia.

Shirika la Manipal Health Enterprise la nchi Uingereza nalo, linaeleza kwamba unapokuwa na ulaji usioleweka kiasi kwamba mwili wako unaongezeka na kupungua mara kwa mara, afya ya nywele zako iko hatarini.

Kwa ujumla, upara sio jambo la ajabu hususan kwa wanaume wenye umri mkubwa. Lakini kama mtu ataanza kupoteza nywele zake mapema, anaweza kuwa na tatizo la kiafya ambalo mara nyingi linahusiana na ulaji.

Ni vyema kuwaona wataalam wa afya hususan waliobobea kwenye lishe ili kujua namna ya kuzuia upara unapotokea katika namna ya kutia shaka.

error: Content is protected !!