Mabasi 41 yafungiwa kusafirisha abiria mikoani

HomeKitaifa

Mabasi 41 yafungiwa kusafirisha abiria mikoani

Jana Novemba 8, magari 41 yalizuiliwa kusafirisha abiria kutokana na hitilafu zilizobainika katika magari hayo kufuatia ukaguzi uliofanyika kwa takribani masaa 6, Ukaguzi huo ulifanyika katika kituo cha mabasi cha Magufuli jijini Dar es Salaam ukiongozwa na mkuu wa usalama barabarani ASP Ibrahim Samwix.

Magari ambayo yalikua na hitilafu za kawaida yalitengenezwa kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari huku yaliokua na hitilafu kubwa yaling’olewa namba za usajili na kutakiwa kupelekwa gereji, ASP Samwix alisema “Walipaswa kuyatengeneza kabla ya kupakia abiria wanayaleta stendi wakifahamu yana hitilafu jambo ambalo hatuwezi kulifumbia macho”.

Mwenyekiti wa chama cha Kutetea Abiria (Chakua) Maulid Bujigwa alisema, “Bahati nzuri hata abiria kwa sasa ni waelewa mwanzo walikua wakichukia na kuona ni usumbufu lakini kuna msemo unaosema kawia ufike, wamekua wakitoa ushirikiano kwa askari hapa kituoni na mabasi yanayofanya ujanja kutaka kuendelea na safari wakati ni mabovu, madereva wake wanakumbana na mkono wa sheria”.

Pamoja na kuendelea kwa ukaguzi katika kituo hicho msimamizi wa mabasi ya kampuni ya Kiteto yanayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Kondoa, aliwekwa mahabusu baada ya abiria kulalamika kuchukuliwa nauli zao na kutofahamu hatma ya safari huku dereva na kondakta wa gari hilo wakitokomea baada ya kuzuiwa kutoka hadi basi litengenezwe.

error: Content is protected !!