Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa tatizo la maji katika miji mikubwa kama Dar es Salaam litaenda kupungua kutokana na jitihada zinazoendelea kufanyika katika bonde la Mto Ruvu.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Ziwa, Bugando Rais Samia ameeleza kuwa jitihada zinazoendelea kufanyika ni pamoja na kuhakikisha maji yote yaliyochepushwa yanarudishwa katika mkondo wake ili kuongeza kina cha maji ambacho kilipungua.
Sambammba na hilo pia ameeleza kuwa Serikali imeendelea kutoa kifusi cha mchanga kilichopo katika mto Ruvu ili maji yaongezeke kwa ajili ya kuchakatwa tayari kusambaza kwa matumizi ya majumbani.
Rais Samia ametaja sababu ambazo zimechangia changamoto hiyo kuwa ni ukaidi wa binadamu kwa kuvamia vyanzo vya maji na kuchepusha maji kwa ajili ya kilimo, akitolea mfano bonde la Ruvu ambapo watu wameweka magogo kupeleka mifugo yao kwa wingi, jambo linalosababisha kuharibu vyanzo vya maji.
Jambo lingine ni ukataji miti na uchomaji miti unaopelekea kutokea kwa ukame pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu. Kukabiliana na changamoto hizo Rais Samia amezitaka kamati za ulinzi za mikoa na wilaya kulinda vyanzo vya maji na kuwachukulia hatua watu wote ambao watabainika wanachepusha maji.
Aidha viongozi wa dini wameombwa kuendelea kuomba mvua za neema zinyeshe katika nchi yetu ambapi maombi ya kuombea nchi mvua yameanza leo mkoani Mwanza.