Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema anashangazwa na diwani mmoja Wilayani Kigamboni (hakumtaja), kwani diwani huyo ameongoza wananchi kugomea mradi wa uchimbaji mchanga uliopo Kigamboni.
Rais Samia ameyasema hayo wakati akishuhudia hafla ya utiaji saini mkataba wa madini baina ya serikali na Kampuni za uchimbaji madini.
“Nina taarifa kwamba ule mradi wa kuchimba mchanga uko Kigamboni, na wakati wa kutambulisha wanachi wa Kigamboni hawapo hapa leo na hawapo kwasababu walishaanza vurugu wakiongozwa na Diwani wao. Na nina alama ya kuuliza na yule Diwani, kwasababu wakati tunafanya operesheni ya wamachinga diwani peke yake aliyeleta vurugu ni huyo wa Kigamboni, aliyepinga wamachinga wasiondoke. lakini wakati wa mradi huu ni yeye ameongoza tena wananchi wa Kigamboni kuanza vurugu” amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu.
Hivyo Rais Samia alitaka wananchi kushirikishwa katika mipango hiyo ya uwekezaji kwani ina manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi kama vile upatikanaji wa ajira, pamoja na hayo miradi hiyo italeta manufaa mengine kama kodi, tozo lakini pia uuzaji wa huduma kwa makampuni.
Pamoja na hayo Wizara ya Mazingira wametakiwa kuja na mipango mikakati ambayo yatasaidia utunzaji wa mazingira maeneo ambayo miradi hiyo inafanya kazi, viongozi pia kuanzia ngazi ya Serikali za mitaa mpaka wabunge wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao na sio kufanya mradi wa kukusanya mapato kwa kuwatoza faini pamoja na kuwapa vitisho wawekezaji hao wa madini waliopo kwenye maeneo yao.