Wajasiriamali wadogo wanavyonufaika na ujenzi wa madarasa na vituo vya afya

HomeKitaifa

Wajasiriamali wadogo wanavyonufaika na ujenzi wa madarasa na vituo vya afya

Utekelezaji wa mradi wa vyumba vya madarasa kupitia fedha za mpango wa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 na ule wa ujenzi wa vituo vya afya kupitia tozo za miamala ya simu umewanufaisha wananchi mbalimbali wakiwemo wajasiriamali wadogo.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 15,000 vya shule za sekondari, mabweni 50 ya watoto wenye mahitaji maalumu wakati vituo vya zaidi ya 200 katika maeneo mbalimbali vikijengwa kwa kutumia fedha za tozo za miamala ya simu zilizopitishwa na Bunge Julai mwaka jana.

Miradi iliyofanyika katika wilaya mbalimbali imeonekana kuleta neema kuanzia kwa walimu, wanafunzi hadi wajasiriamali wadogo wakiwemo mama lishe waliokuwa wakitoa huduma za vyakula kwa mafundi waliokuwa wakijenga vyumba vya madarasa na vituo vya afya.

Baadhi ya kina mama lishe katika halmashauri mbalimbali waliishukuru Serikali kwa kutekeleza miradi hiyo, wakisema imewasaidia kuwaingizia kipato cha muda mfupi kilichowasaidia kujikwamua kiuchumi na kimaisha.

Wanufaika wa mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa, ofisi za walimu pamoja na  vituo vya afya walieleza hayo hivi karibuni wakati wakielezea umuhimu wa mradi huo wakisema licha ya mchakato huo kuwapunguzia adha wanafunzi lakini pia umewakwamua kiuchumi.

Bituni Said aliyekuwa akitoa huduma ya chakula kwa mafundi waliokuwa wakijenga vyumba vya madarasa na ofisi za walimu za shule ya sekondari ya Mwisho wa Shamba iliyopo halmashauri ya wilaya ya Korogwe, aliishukuru Serikali kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi huo.

“Baada ya Serikali kuanza mradi huu, nilifanikiwa kupata zabuni ya kuwalisha mafundi waliokuwa wakitekeleza mchakato huu. Nashukuru Mungu, nilipata fedha zilizomsaidia mwanangu anayesoma Chuo Kikuu  cha Tumaini -Iringa na yule  wa kidato cha nne.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuteleza mradi huu, kwa kutumia mfumo wa mafundi wa ndani ambapo baadhi ya vijana wanaozunguka eneo hili walipata vibarua,” alisema Bituni.

Naye Rose Daudi aliyekuwa akitoa huduma ya chakula kwa mafundi waliokuwa wakitekeleza ujenzi wa kituo cha afya cha Kwafungo wilayani Muheza chenye thamani ya Sh250 milioni, aliishukuru Serikali akisema uwepo wa mradi huo umenufaisha kiuchumi.

“Nakuja hapa nawaletea chakula cha mchana mafundi hawa, kiukweli nashukuru Mungu, napata fedha za kujikimu kimaisha. Ujenzi huu umetunufaisha hadi sisi watu wa chini, tunamshukuru Rais Samia,” alisema Rose.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri wa wilaya ya Muheza, Nassib Mmbaga alisema asilimia 40 hadi ya 50 ya fedha zaidi ya Sh1.4 bilioni za mradi huo, zimebaki wilayani humo. Alifafanua kuwa mafundi, vibarua na mamalishe waliokuwa wakitoa huduma katika miradi hiyo walitoka Muheza.

“Fedha hizi zimetoka Serikalini na kuwanufaisha wananchi wote. Fedha hizi zimeondoa umasikini usio wa kipato  kwa sababu umewapatia elimu, lakini kupata kwao elimu kumesaidia kuondoa umasikini wa kipato walichokipata moja kwa moja kupitia shughuli walizozifanya.

“Ni ngumu watu kuliona hili, lakini fedha hizi zimefanya kazi zote kuondoa umasikini usio wa kipato na kuondoa umasikini wa kipato. Mafundi na vibarua walikuwa 638 wakiwemo kina mama na hizi fedha walizolipwa zinashuka hadi chini wanakopata mahitaji mbalimbali,” alisema Mmbaga.

error: Content is protected !!