Historia imeandikwa tena nchini Tanzania kwa namna ambavyo Dkt. Tulia Ackson ameibuka mshindi wa nafasi ya spika kwa kupata kura 376 sawa na 100% ya kura zote 376 zilizopigwa, jambo ambalo halijawahi kutokea nchini na kumfanya kuwa Spika wa pili mwanamke kuliongoza Bunge hilo.
Jambo pekee lililompa ushindi Tulia ni uzoefu tofauti alioupata kuliko wagombea wengine aliokuwa akishindana nao katika kuwania nafasi hiyo ya Spika. Siri pekee ni uzoefu alioupata wakuliongoza Bunge mwaka 2015 miezi michache baada ya uchaguzi , Spika mstaafu Job Ndugai kupata changamoto za kiafya hivyo ilimlazimu Tulia kushika madaraka na kuanza kutekeleza majukumu kama Spika.
Hivyo basi, kwa uzoefu huo ni dhahiri kuwa wabunge wanaimani na Dkt. Tulia kwamba ataliongoza Bunge hilo vyema kwani kwa muda mrefu amekuwa akitumikia kiti cha Unaibu Spika pamoja na nafasi yake ya Ubunge akiwakilisha jimbo la Mbeya Mjini.
Dkt. Tulia alipokuwa akinadi sera zake aliahidi kufanya kazi bila kujali chama wala kupendelea pande fulani kwakusema kwamba Bunge hilo lipo kwa ajili ya kuwasilisha changamoto na kutatua vikwazo vinavyo wapata wananchi wa Tanzania nzima kwa kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.