Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amefanya mazungumzo na Uongozi wa vilabu vya Atletico Madrid na Getafe vinavyoshiriki Ligi Kuu ya Hispania (Laliga) kwa lengo la kuitangaza Tanzania hususani sekta ya utalii.
Mazungumzo hayo yameonyesha mwanga kwani vilabu hivyo vimeonyesha utayari wake wa kushirikiana kuitangaza Tanzania, Matangazo hayo yanategemewa kuwekwa kwenye jezi za vilabu pamoja na mbao za matangazo (Billboards) zilizopo uwanjani.
“Shabaha yetu kubwa kama nchi ni kuhakikisha tunafungamanisha utalii na michezo kwa kutumia timu kubwa za mpira kwa lengo la kuwavutia watalii wengi zaidi kuja nchini Tanzania” amesema Dk Ndumbaro.
Aidha Dk Ndumbaro amesema kuwa Tanzania inategemea utalii wa wanyama pori kwa asilimia 100, hivyo mkakati huo utasaidia kutumia michezo ili kutangaza vivutio vingine vya utalii kama vile utalii wa fukwe, utalii wa utamaduni pamoja na utalii wa ikolojia utaweza kujulikana na dunia kote na hivyo watalii kuanza kumiminika.
Ujumbe kutoka Tanzania ulioenda Spain kwaajili ya Mazungumzo hayo uliongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Uhispania mwenye makazi yake mjini Paris, Ufaransa, Samwel Shelukindo.