Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amezielekeza shule zote za sekondari ndani ya Jiji la Dodoma kufunga kamera za usalama (CCTV) kusaidia kubaini watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu katika maeneo ya shule.
Alitoa maelekezo hayo jijini hapo alipokuwa akizungumza na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Miyuji iliyopo Kata ya Mnadani jijini Dodoma. Alitembelea shule hiyo kutoa pongezi kwa Bodi na uongozi wa shule hiyo kutokana na kuweka mfumo wa kamera za usalama kwa ajili ya ulinzi na usalama.
Alisema kumekuwapo na matukio mengi ya uhalifu katika Jiji la Dodoma ikiwa ni pamoja na vitendo vya wizi na uharibifu wa miundombinu kutokana na kasi ya ukuaji wa jiji.
“Nitoe pongezi kwa bodi ya shule pamoja na uongozi wote kwa ujumla kwa kushirikiana mpaka kuweka mfumo wa CCTV Camera, hili ni jambo kubwa sana, mmejiwekea ulinzi na wahalifu wataonekana,” alisema.
Alitaja matukio ambayo yamekuwa yakibainika kuwapo kwenye shule kuwa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu hususani milango ya madarasa na madawati kuibiwa.