Bara la Afrika lina historia ya muda mrefu na mashujaa wengi ambao tumekuwa tukiwasoma shuleni na vyuoni. Lakini mara nyingi tumekuwa tukisoma au kusikia historia za mashujaa wanaume, jambo ambalo limekuwa likituacha na kiu ya kutaka kujua mashujaa wanawake waliobeba historia ya bara hilo.Basi leo yawezekana kiu yako tukaipunguza kwa kukutanisha na mwanamke shujaa na jasiri kutokea barani Afrika.
Namzungumzia malkia Amina wa ngome ya Zazzau kutoka nchini Nigeria ambaye katika historia nchini humo anajulikana kama mwanamke mwenye uwezo kama mwanaume.Historia ya shujaa huyu tutaifahamu kupitia filamu ya Amina, iliyoigizwa kwa ufundi na ladha ya kiafrika yenye kuvutia kutazama na kukufanya kuelewa vema historia hii.Historia ya malkia huyu inatufanya turudi nyuma miaka 500 iliyopita, ambapo Amina akiwa ni ‘princess’ mdogo mwenye ujasiri na kipenzi cha baba yake.
Amina yupo katika kipindi ambacho mwanamke hana sauti wala maamuzi yeyote mbele ya mwanaume zaidi ya kudharaurika na kunyanyasika. Licha ya hayo binti huyu mdogo haogopi chochote na zaidi anamuomba mfalme apate mafunzo ya upiganaji na kutumia silaha kama wapiganaji wengine katika ngome yao. Jambo analoomba Amina kwa baba yake siyo tu linavunja mila na desturi za Zazzau bali linaweka ufalme wa baba yake hatarini.
Mapenzi ya mfalme kwa binti yake huyu yanafanya kutokujali yote hayo na kwa mara ya kwanza katika ngome ya Zazzau mwanamke anaingia katika mafunzo ya kupigana na kutumia silaha.Nikwambie tu, hapo ndipo safari ya kishujaa ya binti huyu jasiri inapoanza. Amina anafanikiwa kuwa mpiganaji matata katika ngome ya Zazzau, na anapokuwa mkubwa anaanza kumsaidia baba yake katika mambo mbalimbali ya kuongoza ngome hiyo.
Ushujaa wa Amina unadhihilika wazi pale anaposhiriki katika vita na kurudi na ushindi unaofanya ngome ya Zazzau kuwa kubwa zaidi. Ujasiri wa Amina na uwezo wa kupigana, unakuwa ni tishio kwa watu wanaotamani kiti cha ufalme, akiwemo Madaki ambaye ni katibu wa mfalme anayeaminiwa sana. Kwa kuchukua hatua zaidi Madaki anaandaa mpango wa kumuangamiza Amina kwa kumtumia wauaji bila mafanikio huku mpango huo ukiondoa maisha ya mdogo wake Zaria.
Uchungu anaoupata Amina wa kumpoteza mdogo wake unamfanya azidi kuwa jasiri, na hasa pale anapotambua kuwa ufalme wa baba yake upo hatarini na ni yeye pekee ndiye mwenye nguvu ya kuwakomboa watu na ngome ya Zazzau.
Ni nini shujaa huyu wa kiafrika atafanya kuikomboa Zazzau? Natamani niendelee kukusimulia lakini nina wasiwasi kwamba nitamaliza uhondo wote.
Nguvu aliyonayo mwanamke katika kuikomboa jamii yake, na hata uwezo wa kuvumilia na kuvuka vikwazo kwa ujasiri ili kufikia malengo yake ni sehemu ya filamu hii iliyobeba historia adhimu, unapitwaje?