Kijana mwenye umri wa miaka 17 kutoka Zanzibar amenusurika kifo baada ya kunywa mafuta ya Taa January 15 mwaka huu baada ya kupata matokeo mabaya ya kidato cha nne, mwanafunzi huyo anadai kuwa alitekeleza tukio hilo kutokana na msongo wa mawazo kwani ni mara yake ya pili kufanya mtihani wa kidato cha nne na kupata matokeo yasiyoridhisha.
Kijana huyo anadai mara ya kwanza alipofanya mtihani wake wa kidato cha nne alipata daraja la nne la ufaulu, baada ya kurudia na kufanya tena mtihani kwenye matokeo yaliotoka hivi karibuni amejikuta amepata C ya Kiswahili jambo ambalo hakulitegemea.
Kamishna wa Polisi na Kamanda Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Abdallah Husein Mussa, alisema mwanafunzi huyo baada ya kunywa mafuta aliishiwa nguvu na kupoteza fahamu, baadaye alikimbizwa hospitali Mnazi mmoja na kupatiwa matibabu.
Kamanda Abdallah alisema tukio lolote la kutaka kujiua ni kinyume na sheria na kwamba jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi litakapokamilika atafikishwa mahakamani.
Mtaalamu wa ushauri nasaha, Asya Saleh alisema elimu ya ushauri nasaha inahitajika kwa wanafunzi shuleni, ili wanapokua na msongo wa mawazo waepuke kuchukua uamuzi mgumu.