Awamu ya 6 na mageuzi Bandari ya Mtwara 2022-23

HomeKitaifa

Awamu ya 6 na mageuzi Bandari ya Mtwara 2022-23

Ile kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya “Kazi Iendelee” sasa inafanya kazi tena kwa kasi sana kwani serikali ya awamu ya sita chini yake inakusudia kutumia bandari ya Mtwara kusafirisha zao la korosho kwenda nje ya nchi katika msimu wa mwaka 2022/23 mara baada ya kukamilika kwa ukarabati wa miundombinu ya bandari hiyo. 

Huenda hatua hiyo ikapunguza gharama za usafirishaji kwa wakulima wa mikoa inayolima zao hilo ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani kwa sababu iko karibu na bandari hiyo. 

Mhandisi Godfrey Kasekenya ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ameeleza hayo leo Juni 21, 2022 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum, Tunza Malapo aliyetaka kujua Serikali ina mikakati gani kuhakikisha bandari ya Mtwara inatumika kusafirisha zao hilo la biashara.

Mhandisi Kasekenya amesema katika kuhakikisha bandari ya Mtwara inatumika kwenye msimu wa korosho unaotarajiwa kuanza hivi karibuni  Serikali  imepunguza tozo za bandari kwa asilimia 30 pamoja na kuondoa gharama za utunzaji wa makasha ya kusafirishia korosho katika bandari hiyo.  

“Kumekuwa na jitihada za makusudi kwanza kupunguza tozo zote za bandari kwa asilimia 30 kwa bandari ya Mtwara tu, lakini pia Serikali imeondoa gharama zote za utunzaji makasha ya kusafirisha korosho katika kipindi chote cha msimu wa korosho ikiwemo na msimu huu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, katika msimu wa 2021/22, uzalishaji wa korosho umefikia tani 238,555.81 sawa na asilimia 85.2 ya lengo la kuzalisha tani 280,000 na ambapo Kati ya kiasi hicho, tani 130,296.9 zimezalishwa Mtwara.

Maboresho bandari ya Mtwara

Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kukamilisha uboreshaji wa miundombinu, ununuzi wa vifaa vipya na kuitangaza bandari ya Mtwara pamoja na kupunguza tozo za mizigo inayosafirishwa kupitia bandari hiyo.

“Serikali imekamilisha uboreshaji wa miundombinu ya bandari ya Mtwara na ununuzi wa vifaa vipya ambavyo vitawasili Agosti 2022 kwa ajili ya bandari ya Mtwara ,…

“Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi ya Bandari (TPA) inaendelea kuitangaza bandari ya Mtwara pamoja na kupunguza tozo za bandari ya Mtwara,’ amesema Kasekenya. 

Tayari bandari hiyo imeanza kusafirisha makaa ya mawe na kampuni ya saruji ya Dangote itaanza kusafirisha malighafi zake. 

Mei 8, 202, meli ya MV Southern Cross ilitia nanga katika bandari ya Mtwara kwa ajili ya kusafirisha tani 69,960 za makaa ya mawe kuelekea barani Ulaya ambapo inatajwa kuwa ndiyo shehena kubwa zaidi kusafirishwa ambapo shehena ya mwisho ilikuwa ni tani 59,815.

 

 

 

error: Content is protected !!