Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ambaye alikuwa kwenye msafara wa waliokwenda kupanda Mlima Kilimanjaro, amesema chanzo cha kifo cha mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), mkoani Manyara Joachim Kapembe ni baiskeli.
Msigwa amesema kwamba Kapembe hakuwa na shida yoyote ya afya kwani ndiye aliyekuwa akirekodi matukio ya upandaji mlima wakati wa kupanda na kushuka.
“Tulipofika Kibo kampuni inayohusika na kuongoza watalii iliandaa kama baiskeli nane kwa ajili ya baadhi ya watu ambao wangetaka kutoka kambi ya Kibo kwenda Horombo waende kwa baiskeli badala ya kutembea, kwahiyo watu wachache walipata baiskeli mmoja wapo ikawa ni yeye Kapembe,
“Sasa wakati anatoka kwenye ule mteremko wa kwanza kutoka kambi ya Kibo unapoelekea Horombo mtelekemko wa kwanza ndipo alipopata ajali ya baiskeli ambayo imesababisha hatimaye kifo chake,” ameeleza Msigwa.
Aidha, Msigwa ameeleza kwamba Kapembe atakumbukwa kwa umahiri wake katika utendaji kazi.