Bandari ya Mtwara kuwa kitovu cha meli kubwa

HomeKitaifa

Bandari ya Mtwara kuwa kitovu cha meli kubwa

Bandari ya Mtwara inatarajia kuwa kitovu cha kupokea meli kubwa za makasha kisha kuyapeleka nchi nyingine kwa kutumia meli ndogo.

Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, James Ng’wandu alisema kujitokeza kwa wafanyabiashara wengi wa kuleta makasha kwenye bandari hiyo kunatokana na punguzo lililotoa bandari hiyo kwa miaka miwili sasa ya kuvutia wafanyabiashara kutumia bandari hiyo.

Miongoni mwa punguzo hilo la kuwavutia wafanyabiashara ni kuongeza muda wa makasha kukaa bandarini bila kutozwa kodi kutoka siku 14 hadi 21 kwa makasha yasiyo na mzigo na siku saba hadi 14 kwa makasha yenye mzigo.

Punguzo lingine lililotolewa na bandari hiyo ni gharama za kuhifadhi mzigo wa kwenye makasha au mazao kulipa tozo ya asilimia 0.5 badala ya asilimia moja.

Pia tozo inayolipwa na mwenye mzigo imepunguzwa kwa asilimia 30 na tozo anayolipa mwenye meli nayo imepunguzwa kwa asilimia 30.

Hatua hiyo ya Bandari ya Mtwara inakwenda sambamba na agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilolitoa la kuitaka ipunguze tozo ili kuvutia wateja.

 

error: Content is protected !!