Watanzania wameshauriwa kutojihusisha na shughuli za kilimo ambazo zinatangazwa na makampuni mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii, kwani kihalisia hakuna shughuli hizo bali ni “utapeli”.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliyekuwa akizungumza na wanahabari, leo Januari 30, 2023 amesema wamekuwa wakipokea malalamiko ya watu kutapeliwa fedha zao ambapo tayari wameshaanza kuzichukulia hatua baadhi ya kampuni zilizojihusisha na uhalifu huo.
“Hakuna kilimo kinachoendeshwa kwa Whatsapp, Facebook wala Twitter, jiepusheni, hamna mtu anaweza kukwambia leta milioni 10 halafu baada ya miezi mitatu njoo chukue milioni 15, kwenye kilimo hakuna ‘shortcut’ (njia ya mkato),” amesema Bashe.
Ushauri huo wa Bashe unakuja kipindi ambacho kumekuwa na mfululizo wa matukio ya watu kutapeliwa nchini Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Hivi karibuni Mbunge wa Buchosa Erick Shigongo alitoa rai hiyo hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ambapo watu wengi walionesha kuguswa na ujumbe wa kiongozi huyo.
Ukisikia kauli hizi:
Njoo tukufugie kuku, tukulimie matikiti, tukufanyie biashara, we kaa tu nyumbani uje kuchukua faida kila mwezi, Usifanye! Huu ni wizi wa kawaida unaitwa “ponzi scheme” wengi wamelia, huwa wanalipwa wa mwanzo tu kuvutia, jiepushe na fedha za mkato! Acha uvivu— Eric James Shigongo (@ericshigongo) January 21, 2023
Hatua zinazochukuliwa
Kwa Mujibu wa Bashe tayari wameshachukua hatua za kisheria kwa kampuni ya Jadeja pamoja na Jatu ambazo wananchi walilalamika kutapeliwa fedha zao kupitia miradi ya kilimo iliyoendeshwa na kampuni hizo ambao kundi kubwa ni waajiriwa katika taasisi mbalimbali.
Pamoja na elimu inayoendelea kutolewa kwa jamii kuhusiana na utapeli huo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetunga sheria na kuanzisha mamlaka itakayoitwa Copra ambayo itakuwa na kazi ya kusimamia na kudhibiti kampuni zinazojihusisha na kilimo.
“Hivi karibuni tutangaza Mkurugenzi mpya wa Copra atakayeshughulikia haya yote, mtu akishasema nalima, nimewachangisha watu hela huyo tutamfatilia kwa ukaribu sana, “ amesema Bashe.