Diamond Platnumz ambaye jina lake halisi ni Nassib Abdul, ni moja ya Mwanamuziki mkubwa barani Afrika na Afrika Mashariki kwa sasa. Nyimbo zake zinasikilizwa sehemu mbalimbali duniani, anapata ‘shows’, amewahi kutajwa na kushinda tuzo mbalimbali.
Maisha ya sanaa hasa muziki ya gharama zake. Waswahili hawakuchelea kusema, “Kwenye riziki hapakosi fitin”.. maana yake ni kwamba fedha huwa chanzo kikubwa cha ugomvi kwa walio wengi. Diamond Platnumz safari yake ya mafanikio imegubikwa na mikasa mingi, ikiwamo kutofautiana mitazamo na watu, maslahi ya kibiashara, mahusiano ya kimapenzi na kadhalika.
Katika maisha yake kama msanii amewahi kuwa na maswahiba wengi, lakini kati yao walishatofautiana kwa sababu mbalimbali. Utafiti wa clickhabari unakuleta ‘Beefs’ kuwa tano za Diamond Platnumz watu aliowahi kuwa nao karibu.
Baadhi ya watu ambao Diamond amewahi kupishana nao ni hawa hapa:
1. Ali Kiba
Ali Kiba aliwahi kueleza kwamba yeye (Ali) ni mmoja kati ya watu waliotoa ruhusa ili Diamond arekodi nyimbo katika studio za Sharobaro zilizokuwa chini ya mtayarishaji wa muziki Bob Junior.
Ali Kiba na Diamond, waliwahi kuonekana kuwa karibu wakati Diamond anaanza kuvuma kwenye muziki, ikiwemo kwenda pamoja nje ya nchi kufany kazi (waliwahi kwenda Dubai pamoja).
Lakini baadae Ali Kiba na Diamond wametajwa kama ‘chui na paka’. Mara kadhaa wamewahi kutoa kauli zilizoonekana kama vijembe.
Vita yao ilianza kuonekana zaidi mwaka 2014, kwenye tamasha maarufu, Fiesta (inayoandaliwa na Clouds), ambapo kambi (Team) za wasanii hao zilianza kuonekana katika vita ya wazi.
Hadi leo, Diamond na Kiba wanaonekana kuwa na upinzani mkali na kutoelewana, licha ya kwamba chanzo haswa cha ugomvj wao hakijulikani.
2. ‘Clouds Media’
Diamond, aliwahi kuwa karibu sana na Clouds ambao walionekana kuratibu shughuli zake mbalimbali.
Ukaribu huo ulionekana zaidi wakati marehemu Ruge Mutahaba aliporatibu shughuli kama ‘Zari White Party’ na ‘Diamonds are Forever’ ambazo ziliongeza nguvu ya Diamond kimuziki.
Lakini baadae nyimbo za Diamond ziliacha kupigwa Clouds (Redio na TV). Diamond na wasanii walioko chini yake, wakawa hawaonekani tena kwenye matamasha ya Clouds.
Mwaka 2018 baada ya tamasha la Fiesta kukwama dakika za mwisho kufuatia kufutwa kwa kibali chake (kibali cha kufanya tukio kwenye viwanja vya Leaders), Diamond aliwechapost kwa haraka video iliyomuonesha akicheka kwa nguvu. Video ile ilitafsiriwa na wengi kama ‘dongo’ kwa Clouds.
Ushirikiano wa Diamond na Clouds umekuwa hafifu kwa kipindi kirefu, japo hivi sasa wanaonekana ‘wakipikika chungu kimoja’.
3. Ommy Dimpoz
Ommy ambaye jina lake halisi ni Omari Nyembo, ni kati ya wanamuziki ambao wamewahi kuwa karibu sana Diamond.
Hata hivyo, walikuja kutofautiana na kurushiana maneno makali, kiasi cha Ommy kutishiwa kufunguliwa mashtaka kwa kile kilichoonekana kwamba alimtusi Mama mzazi wa Diamond. Hiyo ilikuwa baada ya Diamond kutoa maneno yaliyomkasirisha Ommy kwenye mahojiano aliyofanyiwa mwezi Agosti 2017 kwenye kipindi cha XXL cha kituo cha redio cha Clouds.
Maswahiba hao wa zamani, hawajawahi kueleza umma iwapo mtafaruku wao ulimalizika, hivyo kama wanacheka baasi wengi wanaamini ‘wanachekeana jino pembe’.
4. Harmonize
Harmonize alikuwa msanii wa kwanza kutangazwa chini ya ‘label’ ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond.
Mwaka 2019 Harmonize aliamua kuvunja mkataba na Wasafi, ambapo ilielezwa kwamba alilipa fedha na kufanikiwa kuondoka ‘WCB’.
Kuvunja mkataba na kuondoka sio ‘bifu’ lakini maneno yaliyofuata baada ya hilo yaliashiria ugomvi.
Harmonize ameonekana kuwa na maneno yanayoaminika kwamba yanamshambulia Diamond kwenye nyimbo zake, na Diamond amesikika mara kadhaa akionesha kwamba Harmonize hakuondoka vizuri ‘WCB’
Kilichoaminika hadi sasa ni kwamba ‘Simba na Tembo’ hawana mahusiano mazuri.
5. Bob Junior (Sharobaro)
Huyu ni mtayaraishaji wa muziki aliyefanya kazi nyingi zilizomtambulisha vyema Diamond.
Alitengeneza wimbo wa ‘Nenda Kamwambie’ ambao ulimtambulisha zaidi Diamond, pamoja na vibao vingine kama Mbagala na Nitarejea.
Baadae Diamond na Bob Junior (Sharobaro Records) wakaingia kwenye mtafaruku ambao pia ulihusisha malipo.
Diamond aliacha kutengeneza nyimbo kwa Bob Junior, wakatengena na hapo ndipo Diamond alipoanza kutumia jina la ‘Wasafi’ ambalo maana yakr haitofautiana sana na Sharobaro (Kwa maana ya utanashati)
Diamond amewahi kuimba kwamba “Muziki vita”, sio ajabu kuwa na ‘bifu’ kwenye muziki. Wakati mwingine ‘bifu’ hizo zimetumika kuongeza umaarufu na faida.
Hata hivyo, ni vyema wanamuziki wakaepuka ugomvi na waamue kushikamana katika kukuza tasnia hiyo.