Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa pamoja wameagiza watendaji wao kuhakikisha wanaondoa vikwazo vya kibiashara kati ya nchi hizi mbili ili kukuza ushirikiano na uchumi wa nchi hizo.
Wizara husika za nchi hizi mbili zimetakwa kufanya hivyo ndani ya mwezi mmoja. Aidha, wamezungumzia kurejeshwa kwa safari kati ya Tanzania na Uganda kwa kutumia Ziwa Victoria.
Kuhusu biashara ya mafuta ghafi Tanzania, itatoza dola 10 kwa kila kilomita 100 kwa lori kutoka Mutukula, Uganda hadi Dar es Salaam, Tanzania kuanzia mwaka ujao wa fedha 2022/2023 unaoanza Julai 1, 2022.
Mapema leo hii Rais Samia Suluhu Hassan ameondoka nchini kuelekea Uganda kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili kuanzia Mei 10 hadi Mei 11, 2022 ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Liberata Mulamula kwa niaba ya serikali amesaini mkataba wa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa nchi hizi mbili.
Rais Samia amesema katika mazungumzo yake ya faragha na Rais Museveni ameweza pia kujifunza mbinu mbalimbali ambazo atazitumia pia kwa nchi yake ili kuleta afueni ya bei ya mafuta Tanzania.
Kwa upande mwingine kutokana na uwepo wa Shule ya Msingi ya Yoweri Museveni, Tanzania (Museveni Pre & Primary School Chato) upo uhitaji wa kupata shule pacha itakayoshirikiana nayo nchini Uganda.
Siku ya kwanza ya ziara ya Rais Samia ikamalizika kwa shukrani hizi.
“Kwa mara nyingine tena namshukuru Rais Museveni kwa niaba ya serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua nzuri ya kujenga shule Chato na kumkumbusha kuwa sasa tunangojea shule dada nchini Uganda mwaka huu,” amesema Rais Samia.