WAKALA wa Maji na Usafi Mazingira vijijini (RUWASA) wilayani Mbogwe imekamilisha mradi mkubwa wa maji uliopo katika eneo la Ushirika-Mlale ambao ulianza kujengwa Aprili 2024 hadi Aprili 2025.
Fedha za mradi huo zimetokana na mfuko wa PforR huku Mkandarasi wa mradi ni Otonde Construction & General Supplies Limited kutoka Mwanza kwa gharama ya Sh bilioni 2,04 pamoja na VAT na amelipwa Sh bilioni 1.84.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbogwe, Mhandisi Rodrick Mbepera ametoa taarifa hiyo mbele ya viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 walipowasili kwa ajili ya kulagua na kuzindua mradi huo.
Amesema mradi huo mkubwa wa maji utanufaisha wananchi takribani 21,009 wa vijiji sita vya Ikobe, Isebya, Ushirika, Mlale, Kadoke na Ushetu ambapo kabla ya mradi kukamilika walikuwa wanatumia maji yasiyo salama.