Rais Samia Suluhu amesema mkutano wa Bunge utakaoanza kesho, pamoja na mambo mengine, utapitia na kupitisha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote uliosubiriwa kwa muda mrefu.
Akihutubia kwenye maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Chama cha Kitume cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema bima ya afya kwa wote itakuwa suluhisho la shida ya kupata matibabu nchini.
“Ninataka niwape habari njema kwamba Bunge litakalokaa mwezi huu wa tisa (Kesho), linakwenda kupitisha sheria ya bima ya afya kwa Watanzania wote. Niwaombe sana ndugu zangu tutakapopitisha sheria hii, Watanzania twendeni tukajiunge na mifuko ya bima.
“Ninataka niwahakikishie kwamba tunajua udhaifu uliopo kwenye mifuko yetu, tumechukua hatua. Tutakapoaanza bima ya afya kwa wote, mfuko utakaosimama kusimamia bima hii utakuwa madhubuti wenye sheria na kanuni mpya ambazo zitafanya watu wote waweze kutibiwa katika viwango mbalimbali.” alisema Rais Samia.