Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa ahadi yake ya kulifufua Jiji na Mkoa wa Morogoro kwa njia ya ujenzi wa viwanda inaendelea kutekelezwa kwa kasi, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Akihutubia wakazi wa kata ya Ngerengere katika muendelezo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, Dkt. Samia amesema kuwa dhamira ya serikali ni kuifanya Morogoro kuwa kitovu cha viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, na maliasili zilizopo katika mkoa huo.
Ameeleza kuwa kazi ya kufufua viwanda imeanza, ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kurahisisha taratibu za usajili wa viwanda, na kuimarisha miundombinu muhimu kama umeme, maji, barabara na reli ili kuvutia uwekezaji wa haraka na wa kudumu.
Kwa mujibu wa Dkt. Samia, utekelezaji wa miradi hiyo utasaidia kuongeza ajira kwa vijana, kukuza kipato cha familia na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla. Amehimiza wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na kulinda amani na utulivu uliopo.
Dkt. Samia ameahidi kwamba serikali ya CCM itaendelea kutoa kipaumbele kwa Morogoro katika mipango ya maendeleo ya viwanda, ikiwa ni pamoja na kusaidia uanzishaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, hasa vinavyomilikiwa na wazawa.