Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema ni muhimu kufufua mchakato wa katiba mpya iili kuendana na mazingira ya sasa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka alisema hayo jana Dodoma wakati akitoa taarifa ya uamuzi wa Halmashauri Kuu CCM Taifa baada ya kukutana.
“Lakini jambo kubwa ningependa nilizungumze kwenu, Chama cha Mapinduzi tunasisitiza umuhimu wa uwepo wa Katiba mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya kwa maslahi mapana ya Taifa na maendeleo kwa ujumla,” alisema Shaka.
Alisema Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM pia imempongeza kwa dhati Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira, maono na kwa uthubutu wa kuhakikisha uwepo wa milango ya maridhiano na kuwaleta Watanzania pamoja.
Shaka pia alisema, CCM inaishauri serikali kuharakisha mambo yote ambayo yatachochea kuimarisha maridhiano ya kisiasa.