Dirisha la maombi ya mikopo kufunguliwa

HomeKitaifa

Dirisha la maombi ya mikopo kufunguliwa

Ikiwa imepita siku moja tu tangu kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita mwaka 2022, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa  Elimu ya Juu Tanzania (HESLB) imetangaza kuwa itafungua dirisha la maombi ya mikopo kwa  wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu hivi karibuni.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru katika taarifa yake iliyotolewa leo Julai 6, 2022 amesema ofisi yake inakamilisha taratibu za uombaji mikopo kwa mwaka 2022/23 na dirisha litafunguliwa katika kipindi cha siku 10 zijazo. 

“Taarifa hii inatolewa kufuatia maombi mengi ya taarifa ya ufafanuzi kutoka kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka 2022 na matokeo yao kutangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) jana, Jumanne Julai 5, 2022,” amesema Badru.

HESLB ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na majukumu ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wanaojiunga na taasisi za elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika.

Badru amewataka waombaji wa mikopo watarajiwa kuwa watulivu na kuanza maandalizi ya awali ya kuandaa nyaraka muhimu kama vyeti vyao vya kuzaliwa, vyeti vya vifo vya wazazi wao vilivyohakikiwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Wakala wa Usajili wa Matukio Muhimu Zanzibar (ZCSRA).

Maelekezo mengine kuhusu mikopo hiyo yataanza kupatikana kwenye tovuti ya HESLB kuanzia Julai 15 mwaka huu. 

“Kuhusu sifa na utaratibu wa kuomba mkopo kwa mwaka 2022/23, maelezo yatapatikana katika Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa mwaka 2022/23 utakaoanza kupatikana katika tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz kuanzia Julai 15, 2022,” amesema Badru.

Katika mwaka wa masomo 2021/22 Serikali ilitenga Sh570 bilioni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Zaidi ya wanafunzi 160,000 wakiwemo wa mwaka wa kwanza zaidi ya 60,000 walinufaika na mikopo hiyo.

error: Content is protected !!