Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amewaambia vijana kuwa Tanzania ni nchi yao, hivyo wasikubali kushawishiwa kuichomoa nchi yao kwa mikono yao wenyewe.
“Msikubali kukata tawi la mti ambao mmeukalia, msikubali kabisa nawaomba mlikatae kwa nguvu zenu zote. Nyinyi ndio walinzi na wajenzi wa Taifa hili, kamwe msije kuwa wabomoaji,”
Dkt Samia ametoa kauli hiyo, leo Ijumaa Novemba 14,2025 wakati akihutubia Bunge jijini Dodoma, ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa Bunge la 13, ambapo pamoja na mambo mengine alitoa mwelekeo wa Serikali yake kwa miaka mitano ijayo.
“Pamoja na kwamba uchaguzi ulifanyika na kumalizika, lakini kulijitokeza uvunjifu wa amani na kuhataarisha amani ya nchi. Niwasihi Watanzania tunapoendelea mbele, tuongozwe na dhamira ya maelewano, ushirikishwa na umoja.
“Kwa wanangu vijana wa Taifa hili, nchi hii imejengwa kwa misingi ya amani na utulivu wa kisiasa.Sisi wazazi wenu tungeshawishika kuyafanya mlioyafanya wakati huu, nchi isingekuwa na neema ya maendeleo mnayoyaona leo,”amesema Dkt Samia na kupigiwa makofi.


