Unakipenda kifo zaidi ya unavyodhani

HomeElimu

Unakipenda kifo zaidi ya unavyodhani

“Enjoy! Maisha ni mafupi” kamsemo wanachoambiwa vijana wengi bila kujua ukubwa wake na namna unavyoweza kugharimu maisha yao.

Utasikia Jamilla anasema ‘najipenda jamani’, ‘ cha kufia nini?’, ‘ya nini nife kwa presha’ na umuhimu wa wa kujipenda lakini matendo yake ni kama analikimbilia kaburi akidhani atakosa nafasi.

Ukijipenda basi utajali afya yako ya mwili na akili, utajali na utakuwa makini kuepuka hatari mbalimbali. Uta’enjoy’ maisha lakini kwa namna itayokufanya uendelee kuyafurahia kwa kipindi kirefu zaidi.

Maisha ni mafupi na kila nafsi utaionja mauti, lakini isiwe sababu ya wewe kuyaishi kwa namna ambayo kesho yako itaumia na kukufanywa ushindwe kukamilisha baadhi ya mipango uliyojiwekea. Yafurahie kwa kiasi ambacho hakitakuweka kwenye hatua ya kuhatarisha maisha yako.

Kijana huna miaka 30, hufanyi mazoezi, unakula vyakula ambavyo vinachochea wewe kupata magonjwa ya moyo, kisukari na hata magonjwa ya moyo. Unakunywa pombe kali kila iitwayo leo na kuvitesa ini na figo yako. Na unajivunia kuwa maji hayapiti kooni asubuhi bila kuzimua kidogo.

Unajua fika kuwa ajali nyingi za barabarani zinazopelekea kupoteza maisha ama vilema vya kudumu kwa sasa ni ajali za pikipiki lakini unapanda pikipiki bila hata kofia ya kulinda kichwa chako. Unaendesha kwa kasi na wala hufuati sheria za barabarani. Huku si kujipenda.

Uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako na huweza kuchochea magonjwa ya mapafu ikiwemo saratani lakini wewe ndio lazima uvute paketi moja kwa siku.

Kujipenda ni pamoja na kuhakikisha unalinda afya yako ili uweze kufurahia maisha kipindi cha uhai wako badala ya kutumia muda mrefu kutafuta dawa na kinga za magonjwa mbalimbali.

error: Content is protected !!