Rais Samia anavyomaliza tatizo la maji nchini

HomeKitaifa

Rais Samia anavyomaliza tatizo la maji nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya na maji katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema anatambua matatizo yanayowakabili kina mama kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo muhimu hivyo Serikali itahahakikisha mpaka kufikia mwaka 2025 tatizo la maji nchini linakuwa limekwisha.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumamosi, Agosti 6, 2022 wakati akizindua mradi wa maji katika kata ya Makongorosi Wilaya ya Chunya wenye thamani ya Sh2.5 bilioni utakaozalisha maji lita Milioni mbili kwa siku.

Amesema katika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ifikapo 2025 ilielekeza kutatua tatizo la maji na kwa Mkoa wa Mbeya kuna miradi 50 ambayo imefikia asilimia 95 na ifikapo 2025 tatizo la maji litakwisha kwa asilimia 100.

”Wito wangu, sipendi kusikia wananchi wanapata maji wakati Rais amefika lakini akiondoka huduma za maji hakuna, Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maji,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Athon Sanga amesema mradi huo umefikia asilimia 70 ambao utazalisha lita milioni mbili zitakazo ondoa tatizo la maji katika Wilaya ua Chunya.

Amesema wizara ina mpango wa kuchimba visima vikubwa vya maji  katika mji wa Makongorosi ili kuondokana na hadha kwa baadhi ya maeneo huku akimpongeza  Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka kwa kutatua changamoto ya maji jimboni kwake kwa kuchimba visima.

Kwa upande wake, Mbunge Kasaka amemuomba Rais Samia kusaidia kuboreshwa miundombinu ya barabara kutoka chunya mpaka kijiji cha Itumbi ambako kuna shughuli za uchimbaji wa madini ili kufungua fursa za kiuchumi.

”Rais Wilaya ya Chunya inategemea zaidi shughuli za uchimbaji madini ambazo zinachochea uchumi tunaomba ikikupendeza miundombinu ya barabara iboreshwe li kuongeza kasi ya shughuli ya uchimbaji wa madini na kuongezeka kutoka kilo 250 mpaka 400 kwa mwezi,”amesema.

 

 

error: Content is protected !!