Kikokotoo cha zamani hakirudishwi

HomeKitaifa

Kikokotoo cha zamani hakirudishwi

Serikali imesema haitarudisha kikokotoo cha zamani cha mafao ya wastaafu cha asilimia 50, kwa kuwa hakileti usawa katika ugawaji wa fedha wanazopata wahusika, pamoja na kuathiri uhimilivu na ukwasi wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako, ameyasema hayo baada ya hoja ya mbunge Mbunge Viti Maalum, Ester Bulaya, ambaye aliitaka serikali iachane na kikokotoo kipya cha asilimia 33, akidai kinawaminya watumishi haki.

Pia alitaka serikali irudishe kanuni iliyokuwa inatoa mafao ya watumishi kwa mkupuo wa asilimia 50.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Ndalichako amesema kikokotoo cha zamani cha asilimia 50, kilikuwa kinawapunja watumishi waliokuwa wanapata mafao ya mkupuo ya asilimia 25.

“Naomba nieleze athari zilizokuwa zinajitokeza kutokana na kanuni za mafao ya mkupuo wa asilimia 50, tunatoa mfano halisi, mchangiaji ambaye amechangia mfuko kwa miezi 467 na michango yake kwa muda wote wa utumishi ni Sh. 36 milioni, kanuni ya zamani ilikuwa inampa mafao ya mkupuo ya Sh. 129 milioni, yaani yeye amechangia Sh. 36 milioni lakini anapata mafao ya mkupuo ya Sh. 129 milioni,” amesema Prof. Ndalichako.

Prof. Ndalichako amesema: “Wafanyakazi wengine ambao wamechangia michango yenye thamani ya Sh. 86 milioni, amefanya kazi miezi 350 kwa kutumia mkupuo wa asilimia 25, anapata mafao ya mkupuo ya Sh. 54 milioni. Huyu amechangia milioni 36 analipwa 129. Huyu milioni 86 analipwa milioni 54.”

Prof. Ndalichako amesema kikokotoo kipya cha asilimia 33, kitaleta usawa kwa mafao ya watumishi: “Wale waliokuwa wanalipwa kidogo watakwenda kupata Sh. 74 milioni kwa kutumia kanuni mpya.”

error: Content is protected !!