Kwa siku kadhaa sasa kumekuwa na mijadala mitandaoni kuhusu masuala ya ufaulu wa wanafunzi vyuoni, mijadala ambayo imeibuliwa na matokeo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo hivi karibuni walitangazwa wanafunzi watatu waliofanya vizuri zaidi. Katika duru ya kwanza ya mahafali hayo kulikuwa na wahitimu wawili wa kike waliopata GPA za 4.7, na duru ya pili kulikuwa na mhitimu wa kiume mwenye GPA ya 4.8, ambayo ndiye alikuwa mwanafunzi bora wa jumla.
Miongoni mwa mjadala huo, ni wazi kwamba baadhi ya watu hawakuwa wanafahmu namna ya kupata GPA, hivyo leo tutaelimishana hatua kwa hatua namna unaweza kupata GPA chuoni.
(a) Jambo la kwanza la kutambua ni kuelewa kila daraja linabeba pointi ngapi katika kutafuta GPA. Daraja A pointi 5, B+ pointi 4, B pointi 3 na daraja C lina pointi 2.
(b) Ili kupata wastani wa namba kadhaa mfano 1,2,3 na 4 unachukua jumla ya namba (1+2+3+4)=10 ambayo unagawanya na idadi ya namba ambazo zipo 4 (jumla/idadi= wastani). Hivyo hapa tutachukua 10/4= 2.5.
(c) Baada ya kujikumbusha hesabu hizi, unapaswa kujua idadi ya kozi zako huko kwa mhula ni ngapi? Kwa mfano tuchukulie kuwa una kozi 5. Chukulia kuwa kozi 1=A, kozi 2=B+, kozi 3+B, kozi 4=C na kozi 5=A.
(d) Kumbuka thamani ya kila daraja (A,B+,B na C) tuliyoyaanisha hapo juu. Angalia una A, B+, B, C ngapi, kisha zidisha hiyo idadi kwa thamani ya daraja husika. Kwa mujibu wa matokeo una A mbili (2×5=10), B+ moja (1×4=4), B mbili (2×3=6) na mwisho C moja (1×2=2).
(e) Kisha jumlisha majibu uliyopata kwa kuzidisha namba hizo katika hatua iliyopita. Hapo utakuwa na hesabu hii 10+4+6+2=22
(f) Katika hatua hii ya mwisho kujua GPA, utachukua jumla ya hesabu ya hatua iliyopita (22) uigawanye kwa idadi ya kozi (5). Jibu hapa litakuwa ni 4.4.
Kwa maana hiyo, GPA yako kwa muhula husika itakuwani 4.4.
Kupata GPA ya mwaka mzima, chukua ya mihula yote, zijumlishe kisha jibu unalolipata gawanya kwa idadi ya mihula husika.
Madaraja ya ufaulu wa GPA kwa Shahada za Awali katika vyuo vikuu Tanzania
Daraja la Kwanza: 4.4 – 5.0
Daraja la Pili la Juu: 3.5 – 4.3
Daraja la Pili la Chini: 2.7 – 3.4
Wamefaulu: 2.0 – 2.6