Faida 6 za Rais Samia kuhudhuria Baraza la Umoja wa Mataifa

HomeKitaifa

Faida 6 za Rais Samia kuhudhuria Baraza la Umoja wa Mataifa

Mkutano wa 76 wa Baraza la Umoja wa Mataifa utaanza rasmi Jumanne Septemba 21, 2021  jijini New York, Marekani,  Makao Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Katika mkutano huo, Tanzania inawakilishwa na  Rais Samia Suluhu Hassan ambaye tayari amewasili nchini humo.
Mara ya mwisho kwa Tanzania kuwakilishwa na Rais kwenye mkutano huo unaokutanisha nchi wanachama 193 ilikuwa ni Septemba 30, 2015, na iliwakilishwa aliyekuwa Rais wa wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
Mwaka 2018, Septemba 28 Tanzania iliwakilishwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi ambaye alihutubia baraza hilo kwa niaba ya Hayati Rais John Pombe Magufuli.
Kuna faida kubwa sana kwa Rais kuhudhuria mkutano huo mwenyewe kuliko kuwakilishwa na mtu mwingine. Kwanza itambulike kuwa, katika taifa lolote lile Rais ndio mwanadiplomasia wa kwanza na mkubwa. Hivyo basi, mwaliko wa mkutano huo huletwa moja kwa moja kwa Rais wa nchi husika, asipohudhuria na kutuma mwakilishi, taswira inayojengeka mara nyingi huwa ni mwaliko huo haukupewa uzito.
Je, kwanini ni muhimu zaidi Rais ahudhurie?
  • Rais anapata fursa ya kukutana na viongozi wa mataifa mbalimbali kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kimataifa baina ya Tanzania na mataifa mengine.
  • Rais akiwa kwenye mkutano huo anapata fursa ya kujifunza na kuwaeleza viongozi moja kwa moja kipi ambacho kinafaa kwa Tanzania na kipi ambacho hakifai.
  • Hata mashirika makubwa ya fedha na misaada, yanakuwa na uhakika zaidi kukutana na Rais wa nchi husika moja kwa moja kuliko kukutana na mwakilishi wake.
  • Rais ana nguvu na kualika uwekezaji, kuomba msaada au mkopo moja kwa moja kutoka kwa mataifa na mashirika makubwa. Hii ni tofauti na mwakilishi, mara nyingi matendo na maneno yao huwa na mipaka kulingana na majukumu yao.
  • Kama Rais alikuwa na ratiba ya kukutana na kiongozi wa taifa lolote baadye, anaweza kutumia fursa katika mkutano huo kukutana nae na akapunguza gharama za kusafiri baadae kwenda kwenye nchi ya kiongozi huyo.
  • Rais pia anaweza kuongozana watu kutoka sekta binafsi nchini au mashirika ya uwekezaji nchini kuelekea kwenye mkutano huo ili kufanya vikao vya kibiashara na uwekezaji.
error: Content is protected !!