Faida za mradi wa kufua umeme wa Kikagati- Murogo kwa Tanzania

HomeKitaifa

Faida za mradi wa kufua umeme wa Kikagati- Murogo kwa Tanzania

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Uganda Yoweri Museveni wamezindua mradi wa kufua umeme wa Kikagati-Murongo (Kikagati Murongo Hydropower Plant), ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 16 za umeme ambazo zitatumika kwa mataifa yote mawili.Mradi huo uliojengwa upande wa Uganda kwa muda wa miaka mitano, umegharimu Dola za Marekani milioni 56 sawa na Sh132.4 bilioni za Tanzania, utategemea maji ya Mto Kagera kuzalisha umeme huo.

Kikagati Murongo Hydropower Plant ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa kupitia uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kushirikisha nchi wanachama ambapo kwa Tanzania mradi huo utazinufaisha baadhi ya wilaya za Mkoa wa Kagera ambazo ni Kyerwa, Karagwe na Misenyi.

Tanzania itakavyonufaika

Rais Samia aliyekuwa akitoa hotuba baada ya uzinduzi amesema mradi huo ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya mataifa hayo mawili ambao utasaidia kukua kwa uchumi kwa jamii za maeneo hayo.

“Jukumu letu kama viongozi wa nchi na Serikali ni kuelekeza uwekezaji kufanyika katika maeneo haya, kama hili tulilopo sasa (mji wa Mbarara uliopo magharibi mwa Uganda), na uwekezaji huo lazima uhusishe uchumi jumuishi ambao utachochea maendeleo,” amesema Rais Samia.

Pamoja na kuimarisha biashara na uwekezaji, mradi huo utaimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo maji safi huduma za usafiri wa abiria na mizigo, upatikanaji wa huduma za afya za uhakika pamoja na kuimarishwa kwa huduma za elimu.

Kuimarisha huduma za mawasiliano

Kukosekana kwa huduma za umeme katika eneo hilo kulisababisha huduma za mawasiliano hususani katika maeneo ya vijijini kuwa hafifu.

Ujio wa mradi huo utakuwa mkombozi ambapo wizara zinazohusika na mawasiliano kutoka Tanzania na Uganda zimeahidi kushirikiana katika kupanua upatikanaji wa huduma hiyo.

Kuongeza ushirikiano wa kijamii na usawa

Faida nyingine inayotajwa ni kuongezeka kwa muingiliano na ushirikiano wa kijamii kati ya mataifa hayo utakaotokana na kuongezeka kwa usalama pamoja na kurahisishwa kwa shughuli za usafiri.

Aidha, shughuli za kiuchumi zitakazoanzishwa kutokana na uwekezaji utakaofanyika kufuatia uwepo wa nishati ya umeme zitachochea ushirikiano huo.

Rais Samia amesisitiza kuwa mradi huo utaongeza usawa kati ya maeneo ya mijini na vijijini kwani wote watanufaika na upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa maendeleo.

Mradi wa Kikagati pia umeijenga upya Shule ya Msingi Murongo upande wa Tanzania kama sehemu Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Ili kuufanya mradi huo kwenda kwa ufasaha Rais Samia ameahidi kushughulikia changamoto zilizobainishwa ikiwemo masuala ya kodi na vibali vya kazi, ambapo tayari Waziri wa Nishati January Makamba amebainisha kuwa zimeshaundwa kamati kutoka kwenye pande zote mbili ili kutatua changamoto hizo.

Kwa upande wake Yoweri Museveni amesema anafurahishwa na ushirikiano unaokua baina ya mataifa hayo na hakutakuwa na kipingamizi iwapo Tanzania itaamua kuununua umeme wote unaozalishwa na mradi huo.

“Kama Tanzania inataka megawati zote kutoka Kikagati, wachukue zote, kwa muda ambao wanaweza kulipia. Sina shida hata kidogo na kusafirisha umeme wetu kwa majirani ambao wanataka kulipia,” amebainisha Museveni.

Tayari mradi unaofanana na huu unajengwa eneo la Rusumo Wilaya ya Ngara. Utazinufaisha nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi wenye megawati 80 na kwa sasa umefikia asilimia 99.

error: Content is protected !!