Falme za Kiarabu na Tanzania kuanza usambazaji wa mbolea kimkakati

HomeKitaifa

Falme za Kiarabu na Tanzania kuanza usambazaji wa mbolea kimkakati

Huenda uhaba wa mbolea unaowakumba wakulima wa Tanzania utapungua siku za hivi karibuni baada ya wawekezaji kuonyesha nia ya kuimarisha mfumo wa usambazaji pembejeo hiyo nchini.

Ofisi ya Sheikh Ahmed Dalmook Al Maktoum, Mwanafamilia ya Kifalme ya Falme za Kiarabu (UAE) imetia saini mkataba wa makubaliano na Wizara ya Kilimo ili kuendesha usambazaji wa kimkakati na uhifadhi wa mbolea kwa ajili ya kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Makubaliano hayo yaliyofanyika jana Februari 25, 2023 yanaonyesha utayari wa kutoa na kusambaza mbolea ya uhakika na yenye ubora kwa Tanzania ili kuchagiza sekta ya kilimo na kuboresha upatikanaji wa chakula kwa wananchi.

Kwa mujibu wa masharti ya makubaliano hayo, ofisi hiyo ya Sheikh Al Maktoum pamoja na washirika wake itaendeleza na kuendesha kituo cha kisasa cha kuhifadhi mbolea nchini Tanzania, ambacho kitakuwa na uwezo wa kufanya usambazaji wa kimkakati wa bidhaa za mbolea.

Jukumu la Serikali ya Tanzania litakuwa kuimarisha miundombinu iliyopo katika maeneo ambayo mbolea itakuwa inasambazwa ili kuwafikia wakulima kirahisi.

Kituo hicho kitawekwa kimkakati ili kuhakikisha kuwa wakulima kote nchini wanapata mahitaji ya mbolea kwa bei shindani.

Ushirikiano huu utasaidia kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanapata mbolea yenye ubora wa hali ya juu ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa mazao na mafanikio ya sekta ya kilimo.

“Tuna furaha kubwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kusaidia sekta ya kilimo nchini,” amesema Sheikh Al Maktoum na kusisitiza kuwa,

“MOU (Makataba wa Makubaliano) hii inawakilisha hatua kubwa ya maendeleo katika juhudi zetu za kuwapatia wakulima nchini Tanzania mbolea yenye ubora wanayohitaji ili kukuza mazao yenye afya na kuboresha maisha yao.”

Ushirikiano huu wa kimkakati utasaidia kukuza ukuaji wa uchumi, kuboresha usalama wa chakula, na kukuza mazoea ya kilimo endelevu nchini.

Ofisi Sheikh Al Maktoum  imedhamiria kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha mpango huu unafanikiwa na inatarajia ushirikiano wa muda mrefu na wenye tija.

error: Content is protected !!