Hapo jana kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomakabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake, kulitokea mvutano wa kisheria kufuatia Mawakili wa utetezi kupinga kupokelewa kwa video sita zilizokuwa kwenye flashi (Flash Disk).
Upande wa Jamhuri ulitaka kuwasilisha flashi hiyo katika ushahidi wa shahidi wake wa nane, Jason Kisaka, lakini upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Mosses Mahuna uliweka pingamizi kwa madai kuwa video sita zilizokuwa ndani ya kifaa hicho, hazikuwa zimeoneshwa mwanzo.
> Sabaya alivyowataja Magufuli na Mpango mahakamani kwenye utetezi wake
“Tumepatiwa vielelezo zikiwamo nyaraka na ‘flash disk’ lakini shahidi amefungua ripoti hiyo ndani ya ‘flash disk’ na ameishia mwanzoni bila kufungua video sita zilizomo humo ndani kwa kuwa hatufahamu zinahusu nini” alisema Mahuna na kusisitiza kwamba Sheria inataka vielelezo vyote vipitiwe kwa mapana yake.
Aliongeza “Tunaomba Mahakama isipokee kielelezo hiki na endapo itakipokea basi shahidi azungumzie sehemu za awali za mafaili ya video hizo na si kuzifungua na kuzungumzia”
Mawakili wa Serikali walidai hakuna utaratibu wa kisheria uliokiukwa kwani Sheria ya Kielektroniki, kifungu namba 15, hakijaeleza kuwa kielelezo kinatakiwa kusomwa ndipo kipokewe Mahakamani.
> Sabaya alivyoachiwa huru na Mahakama kwa kujifanya Afisa usalama
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Othmed Mtega alisema “Tunaiomba Mahakama kupokea kielelezo hiki kwa kuwa shahidi ameeleza kwamba anakifahamu. Pia hoja ya kusema kielelezo kionyeshwe nini kilichomo ndani ni sawa na kukifungua kabla ya kupokewa kwanza kwa kuwa kiutaratibu kinatakiwa kupokewa ndipo kisomwe mahakamani”
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha Patricia Kisinda aliahirisha kesi hiyo Novemba Mosi mwaka huu saa 3:00 asubuhi.