Ushahidi wa maboksi ya fedha kwenye kesi ya Sabaya

HomeKitaifa

Ushahidi wa maboksi ya fedha kwenye kesi ya Sabaya

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, imepokea video sita zilizokuwa kwenye ‘flash disk’ iliyowasilishwa kama ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya, Lengai Ole Sabaya na wenzake.

Wiki iliyopita, upande wa utetezi ulipinga kupokelewa kwa video hizo kama ushahidi katika kesi hiyo lakini baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote, imekubali kuzipokea.

Katika video hizo, watu wawili wanaonekana wakiingia katika benki ya CRDB tawi la kwa Morombo mkoani Arusha na kuchukua maburungutu ya fedha ambazo ziliwekwa kwenye maboksi.

Afisa wa benki alionekana akiwa ameshika maboksi mkononi kabla ya kuanza kuhakiki fedha hizo na kuzipanga kwenye maboksi, kisha aliziweka juu ya kiziti chenye matairi na kwenda kuwakabidhi watu hao wawili.

Watu hao ambao mmoja anaonekana ni mtu wa makamo aliyevaa koti kubwa na mwingine ni kijana, walichukua maboksi hayo yenye fedha na kwenda kuingia nayo kwenye gari la bluu.

Video hizo zilitolewa kama sehemu ya ushahidi wa upande wa Jamhuri kupitia shahidi wake wa nne, Jonson Kisaka.

error: Content is protected !!