Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imesema kwamba, baada ya filamu ya Royal Tour kuzinduliwa katika miji ya New York na Los Angeles Marekani, gari lililoonekana likiendeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan limekuwa kivutio kipya cha utalii katika Hifadhi ya Serengeti.
“Baada ya uzinduzi wa filamu watalii wengi wa ndani na nje ambao wamepata bahati ya kuliona gari hili ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wamekuwa na hamasa na msisimko mkubwa wa kuliona gari hilo lililotumiwa na Rais kwenye filamu ya Royal Tour,”ilieleza taarifa ya Tanapa.
Gari hilo aina ya Toyota ambalo kwa sasa linauzwa sh198.9 milioni limewahi kutumiwa na viongozi mbalimbali walipotembelea hifadhi hiyo, akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete.
Taarifa kutoka Tanapa inaeleza kwamba maandalizi yalihusisha marekebisho ya friji ili kufanya kuwa na vinywaji baridi,maboresho ya siti na kuweka red carpet ili kuwa na muonekano wa ki VIP, kuongeza nafasi na kulinganisha na mazingira na Rais Samia ndiye aliyelichagua.