Hali ya Corona nchini

HomeKitaifa

Hali ya Corona nchini

Wizara ya Afya inaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu hali ya ugonjwa wa UVIKO-19 nchini. Itakumbukwa kuwa ugonjwa huu ulitolewa taarifa kwa mara ya kwanza hapa nchini mwezi Machi 2020 ambapo hadi tarehe 04 Mei 2022 kumekuwa na jumla ya watu 33,916 waliothibitika kuwa na UVIKO-19 na vifo ni 803.

“Idadi ya visa vipya imekuwa ikipungua, ambapo visa vipya vimepungua kutoka 116 kwa mwezi Machi 2022 hadi kufikia 68 katika mwezi Aprili 2022. Katika mwezi Aprili 2022, kumekuwa na ongezeko la wagonjwa kutoka watu nane (08) wiki ya tatu hadi 32 katika wiki ya nne. Hakuna kifo chochote kilichotolewa taarifa katika kipindi cha mwezi wa Aprili 2022 hadi tarehe 4 Mei 2022.”

“Katika kipindi cha tarehe 02 Aprili hadi 4 Mei 2022, jumla ya wagonjwa wapya waliolazwa ni wawili (2) tu, na wote hao walikuwa hawajapata chanjo ya aina yoyote dhidi ya UVIKO-19. Aidha, katika kipindi hicho, hapakuwa na mgonjwa yeyote mahututi kati ya waliolazwa. Vile vile, Wizara inaendelea kufuatilia mwenendo wa ugonjwa hususan kuhusu ongezeko la visa katika wiki ya nne ya mwezi Aprili 2022 na kuchukua hatua stahiki,” imesema taarifa hiyo.

Aidha, Wizara inaendelea kutoa tahadhari kwa wananchi wote kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na kuzuia ugonjwa wa UVIKO – 19 ikiwa ni pamoja na, Kupata kwa wakati dozi kamili za chanjo ya kujikinga na ugonjwa huu, Kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, Kuvaa barakoa kwa usahihi na wakati wote unapokuwa kwenye maeneo yenye mikusanyiko, Kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kitambaa safi, Kuzingatia usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi (sanitizer) mara kwa mara, Kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya endapo utakuwa na dalili za ugonjwa huu, Kuendelea kuchukua hatua za kujenga mwili imara kwa kufanya mazoezi na kula vyakula bora na Kutoa taarifa za kuwepo watu wenye dalili za ugonjwa huu katika jamii kupitia namba ya simu ya bure 199.

error: Content is protected !!