Mkuu wa mkoa Dar es Salaam , Amos Makalla amekiri kwamba hali bado si shwari na kilichopo ni kuomba kudra za Mwenyezi Mungu baada ya kutembelea mto Ruvu kwani mkoa wake unategemea maji kutoka mto Ruvu chini huo uliopo Bagamoyo na mto Ruvu juu uliopo Kibaha.
“Yale ya binadamu tumeshafanya kwa uwezo wetu, ikiwamo kuwasaka wachepushaji maji, kilichobaki ni kudra za Mungu. Tumekuja hapa kuona hali halisi ili mkoa uwe mabalozi wazuri wa kuwaeleza wananchi nini kinachoendelea, kwani ukiona kitu kwa macho ni rahisi kuwaeleza watu kuliko kuelezwa,”alisema Makalla.
Pia alisema chanzo kikuu cha maji katika mto huo ni mvua ambazo zilikuwa zinategemewa kunyesha oktoba na Novemba, lakini hazijaonekana hivyo kutoa funzo kwa wananchi kuwa wanapaswa kutunza vyanzo vya maji na kuyatumia yaliyopo kwa uangalifu.
“Leo tumeona, kuna upungufu wa maji hadi mashine zinatumika kuyavuta, hivyo itabadilika tu pale mvua zitakapoanza kunyesha. Sala ni muhimu , viongozi wetu wa dini waendelee kuomba kwani tulipofika mambo yapo nje ya uwezo wa kibinadamu,”
“Tuombe hali ibadilike kuanzia Novemba hii, Desemba mpaka January. Viongozi wa Dar es Salaam tunaotumia maji haya tumejionea ukweli twendeni tukawaelimishe watu,” alisema Makalla mbele ya wakuu wa wilaya za Dar es Salaam alioongozana nao pampja na waandishi wa habari.