Fahamu kuhusu mlipuko wa surua nchini

HomeKitaifa

Fahamu kuhusu mlipuko wa surua nchini

Serikali ya Tanzania imetangaza kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa surua katika halmashauri saba huku watu 54 wakiwa wemethibitika kukumbwa na maradhi hayo yasiyokuwa na tiba ambayo miongoni mwa dalili ni kutoka upele na kikohozi.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewaambia wanahabari jana Septemba 15,2022 jijini Dodoma kuwa uchambuzi wa majibu ya vipimo vya sampuli za kipindi cha Julai hadi Agosti  umeonesha kuwa halmashauri saba zimekidhi vigezo vya kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo.

Halmashauri hizo zina wagonjwa 38 waliobainika ambapo Bukoba ina wagonjwa watatu, Handeni (wagonjwa  wanne), Kilindi (wagonjwa watatu), Mkuranga (wagonjwa wanne), Manispaa ya Kigamboni (wagonjwa nane), Temeke (wagonjwa 12) na Ilala yenye wagonjwa wanne. Kati ya halmashauri hizi saba, tatu zipo Dar es Salaam.

Ugonjwa huo ambao bado hauna tiba maalumu, kwa mujibu wa Mwalimu dalili zake  kuu  ni homa na vipele ambayo huambatana na mafua au kikohozi, macho kuwa mekundu pamoja na vidonda mdomoni.

Mbali na halmashauri hizo saba, waziri huyo amesema ugonjwa huo meripotiwa katika maeneo mengine ambayo idadi ya wagonjwa waliopo haijakidhi kutangazwa uwepo wa mlipuko. Idadi ya wagonjwa waliopo kwenye maeneo mengine inafanya jumla ya watu walioathiriwa na Surua Tanzania kufikia 54.

“Kwa kipindi cha Julai hadi Agosti 2022  tumethibitisha kuwa na wagonjwa 54, hata hivyo hakuna kifo kutokana na ugonjwa huo,wagonjwa 48 walikua na umri usiozidi miaka 15 na wagonjwa sita walikuwa na umri zaidi ya miaka 15,” amesema Mwalimu.

Halmashauri ambazo hazijathibitika kuwa na mlipuko wa Surua kutokana na kutokuwa na sampuli tatu au zaidi zenye ugonjwa huo lakini kuna wagonjwa ni Arusha, Chalinze, Igunga, Kahama MC, Kalambo, Kigoma DC, Kwimba DC, Masasi Mji.

Ili kuudhibiti ugonjwa huo Waziri Mwalimu amesema wameimarisha ufuatiliaji wa wahisiwa katika vituo vya afya kuanzia ngazi ya jamii, kutuma timu za wataalamu katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi pamoja na kutoa elimu ya ugonjwa huo ikiwemo dalili na jinsi ya kujikinga.

Wazazi wameshauriwa kuwapeleka watoto wao hospitali ili wapatiwe chanjo ya ugonjwa wa Surua ambao dalili zake kuu ni kuwa na homa na upele mwilini.

Surua ni miongoni mwa magonjwa ya kuambukiza ambayo bado yanausumbua ulimwengu ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya la Duniani (WHO) watu 207,000  walifariki kutokana na ugonjwa wa surua mwaka 2019.

error: Content is protected !!