Historia fupi ya Mwai Kibaki kwenye siasa

HomeKitaifaKimataifa

Historia fupi ya Mwai Kibaki kwenye siasa

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, leo Aprili 22 ametangaza msiba wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa nchi hiyo, Emilio Mwai Kibaki kilichotokea leo akiwa na miaka 90.

Kibaki aliapishwa kuwa Rais wa Kenya Desemba 2002 na kuiongoza nchi hiyo hadi mwaka 2013. Alijulikana kama mwanasiasa asiye na kelele nyingi bali matendo.

Kati ya kazi kubwa alizofanya ni kuinua uchumi wa nchi hiyo na kutoa elimu bure mara tu alipoingia madarakani.

“Baada ya kuchaguliwa 2002 alifanya mkutano wa waandishi wa habari wa ambao ulikuwa wa kubadilishana mawazo ya kweli. Sote tulimuuliza ni lini atatoa ahadi za elimu bure kwa shule za msingi – alisema Jumatatu, na mkutano na waandishi wa habari ulikuwa Ijumaa alasiri. Jumatatu iliyofuata, maelfu ya watoto walikuja wakidai masomo ya bure, ameeleza Mhariri Mkuu wa The Africa Report Patrick Smith.

Kibaki ni Rais aliyependwa sana na Kenya kwani aliingia madarakani na kuikuta Kenya kwenye hali mbaya sana kiuchumi lakini aliweza kuisaidia kukuza uchumi huo maradufu katika kipindi cha miaka 10 madarakani.

Akiwa kwenye miaka ya 30, Kibaki alikuwa akishika nafasi kubwa kwenye uchumi wa nchi hiyo.

“Mchango wake kwenye Wizara ya Fedha na kama Makamu wa Rais wa Kenya ulisaidia uchumi wa nchi ukikua kwa kasi,” ameeleza Rais Kenyatta.

Hii ilitokana na uzoefu wake kiuchumi. Kibaki aliwahi kuwa mhadhiri msaidizi somo la uchumi katika Chuo Kikuu cha Makerere lakini pia kuwa waziri wa fedha na mipango ya kiuchumi.

Ni Rais wa kwanza wa Kenya kutoka chama pinzani. Alianzisha chama chake cha Democratic Party baada ya kukorifishana na aliyekuwa Rais kipindi hicho, Daniel arap Moi.

Kutokana na mahusiano yake mazuri na Tanzania pamoja na uongozi imara, Februari 2013 Rais Kibaki alifanya ziara yake ya mwisho  Tanzania akiwa Rais ikiwa ni pamoja na kuwaaga Watanzania kwani alikuwa akiondoka madarakan mwezi uliofuata.

Ziara hiyo ilitamatishwa na uzinduzi wa Barabara ya Mwai Kibaki ambayo inapita Mikocheni, na ni kiunganishi cha nyumba za makazi za Marais wa awamu ya kwanza hadi nne wa Tanzania.

Rais Kenyatta ametangaza maombolezo ya kitaifa kuanzia sasa na chanzo cha kifo chake bado hakijawekwa wazi.

error: Content is protected !!