Historia yaandikwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mtwara

HomeKitaifa

Historia yaandikwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mtwara

Huduma za kibingwa za Taasisi ya tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) zimeanza kutolewa katika hospitali mpya na ya kisasa ya rufaa ya kanda kusini Mtwara ambapo kwa mara ya kwanza historia imeandikwa kwa mgonjwa wa kwanza kufanyiwa upasuaji katika hospitali hiyo.

Upasuaji huo wa kibingwa wa Mifupa umefanywa na jopo la madaktari bingwa ,wauguzi na wataalam wa usingizi kutoka MOI kwa kushirikiana na wataalamu wa hospitali ya Rufaa ya Kusini Mtwara.

Kiongozi wa jopo la wataalamu kutoka MOI, Dkt. Albert Ulimali amesema jopo la wataalam 11 limepiga kambi ya siku tano katika hospitali ya kanda Mtwara kwaajili ya kutoka huduma za kibingwa za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ikiwa ni pamoja na kuwafanyia upasuaji wagonjwa.

“Tuko hapa katika hospitali ya kanda kusini, tumetumwa na kiongozi wetu wa MOI Dkt. Respicious Boniface tuje kuanzisha huduma zetu hapa, tunashukuru muitikio wa wananchi umekua mkubwa ambapo kwa siku ya kwanza peke yake tuliwahudumia zaidi ya wagonjwa ya 280” Alisema Dkt. Ulimali

Dkt. Ulimali amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa hospitali kanda kusini pamoja na usimikaji wa vifaa vya kisasa. Pia amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmad Abass pamoja na Mkuu wa Wilaya Mtwara Mh Dunstan Kyoba kwa mapokezi mazuri.

Daktari bingwa wa Mifupa kutoka MOI, Dkt Tumaini Minja amesema upasuaji wa kwanza katika hospitali hiyo umefanyika kwa mafanikio makubwa na huduma hizo zitaendelea kupatikana hospitalini hapo hivyo wakazi wa mikoa ya kusini wajitokeze kupata huduma.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kusini Mtwara Dkt Jeofrey Ngomo ameishukuru Taasisi ya MOI kwa kusogeza huduma za kibingwa kwa wakazi wa mikoa ya kusini ambapo waogonjwa hawatalazimika kufuata huduma hizo Dar es Salaam.

error: Content is protected !!