Jifunze njia 5 za kuishi na mtu mwenye hasira za karibu

HomeElimu

Jifunze njia 5 za kuishi na mtu mwenye hasira za karibu

Pengine unaogopa kuishi au hata kuzungumza na mtu ambaye unajua ni mwenye hasira za karibu au ni rahisi kukasirika. Kwa usalama wake na wako, mara nyingine unaweza kuamua kutokujikurubisha nae ili kuepusha matatizo ambayo yanaweza kujitokeza. Hasira za mtu juu yako zinaweza zisisababishwe na wewe, bali unaweza ukawa kigezo cha yeye kukasirikia kwa muda huo.

Mtu mwenye msongo wa mawazo au historia mbaya katika maisha yake, anaweza kuwa mtu wa hasira au mwenye kuweza kukasirishwa na vitu vya kawaida katika wakati usioutegemea. Si kila mara suluhisho bora ni kumtenga mtu mwenye hasira, la hasha! zipo namna ambazo unaweza kujifunza na kuweka kuishi na mtu mwenye hasira kali.

1. Tambua vitu asivyopenda
Ikitokea unaishi na mtu mwenye hasira za karibu kwenye nyumba moja, rafiki yako, mke au hata ndugu yako, ni vyema kutambua ni mambo gani humkasirisha kwa wepesi. Unaweza kukaa nae chini na kulizungumza jambo hilo kwa uwazi, hii inaweza kusaidia zaidi kutatua tatizo hilo baada ya muda fulani endapo mtahusisha jambo hilo kwenye mazungumzo. Ni vyema mtu kuzungumza na kupata uvumbuzi wa tatizo linalomsibu. Pia hii itakusaidia kutofanya jambo ambalo unajua fulani halimfurahishi.

2. Wape nafasi
Ikitokea tayari mtu huyo amepandwa na hasira, ni vyema ukakaa nae mbali kwa muda huo. Kumkurubia au kumzungumzisha kunaweza kukaleta matokeo mabaya zaidi. Kumuacha mtu amalize hasira zake mwenyewe kuna uwezekano mkubwa wa yeye kutambua endapo ana makaso, na ni rahisi sana kujirudi kuomba msamaha.

3. Kuwa mstahamilivu
Inapotokea umeingia katika mtafaruku na mtu mwenye hasira kali, na unatambua shida yake, uungwana ni kuwa mstahamilivu. Si vyema kujibizana nae hata kama utahisi ni yeye ndiye mkosaji. Uungwana ni kumuacha amalize na utuame munkari wake, hapo unaweza kumsogelea na kumuweka sawa. Hasira ni kama kilema vile, ni aghalabu kwa mtu mwenye nazo kwa wingi kuweza kuzidhibiti.

4. Toa msaada wa ushauri
Unapotambua kuna mtu wa aina hii, ni bora kumsaidia kuondokana na hali hiyo. Zipo namna mbalimbali za kupunguza hasira ambazo unaweza kumshauri mtu afuate kama vile kufanya tahajudi (meditation) au kufanya mazoezi mara kwa mara. Lakini pia kama unafahamu mtu huyo anakipaji kama cha muziki au kuchora, ni vyema ukamshauri akawekeza muda wake mwingi huko kwani inaweza kumsaidia kupunguza hasira.

5. Jitathmini
Matatizo yanaweza kuanzia kwako na unaweza kuwa chanzo za kusababisha mtafaruku. Tazama kauli zako na tabia yako kwa ujumla kisha jidhibiti ili usiwe chanzo cha matatizo. Si kila muda watu wenye hasira wanaweza kuwa chanzo cha mgogoro, lakini hata watu wanaowazunguka, ukiwamo wewe unaweza kuwa chanzo cha mgogoro. Hivyo ni vyema kujitathmini mara kwa mara na kutambua tabia za watu wengine na kujua namna ya kuishi nao bila kuingia kwenye mikingano isiyo ya lazima.

error: Content is protected !!