Utanashati na umaridadi wa mtu huletwa na muonekano wake wa nje kwanza kuanzia usafi wa mwili hadi mavazi aliyovaa na muonekano wa mavazi hayo.
Unaweza kuvaa shati la gharama, lililofuliwa vizuri lakini kama halijapigwa pasi na kunyooka vizuri, lakini bado usiwe nadhifu.
Kupiga pasi imechukuliwa kana kwamba ni kazi ya mtu kujifunza kwa namna yake mwenyewe na anaweza kupasi kwa namna yeyote ile suala ambalo si sahihi, kwani kupasi, hasa mashati huhitaji umakini, uzoefu na ujuzi wa hali ya juu kulingana na aina ya kitambaa cha nguo unayopasi lakini pia aina ya pasii unayotumia.
Unapoanza kupasi shati, hakikisha umefungua vifungo vyote vya shati lako. hii hukupa urahisi wa kuweza kupasi shati na kuzifikia kona zote bila tatizo.
Toa vipande vya plastiki ngumu ambavyo huwekwa kwenye ukosi wa shati lako hasa kwenye mashati ya kiume ili kuzui ukosi kujikunja
Usipasi nguo zikiwa kavu, tumia chupa ya kunyunyiza maji, kama hauna pasi yenye kunyunyiza maji. Unapopasi nguo zikiwa hazina unyevu unasababisha zipauke na kupoteza rangi yake, lakini pia ubora wa kitambaa unaanza kupungua taratibu.
Anza kwa kupasi ukosi kutokea kwenye kona mbili kwenda katikati ili kona zisijikunje kisha mikono. Fungua vifungo vyakwenye kiwiko na upasi kuanzia katikati ili kitambaa kisijikunje kutengeneza mistari midogo midogo kisha kama ulibyofanya ukosi anza kupasi tena kutoka kwenye kona kurudi ndani.
Hatua inayofuata ni kunyoosha upande wa nyuma wa shati kwa kuanzia na kile kipande kilichopo shingoni kinachojulikana kama ‘yoke’ nyoosha kutoka nje kwenda ndani. Ukimaliza sasa unaweza kupasi upande wote wa nyuma wa shati lako.
Geuza shati mbele upande wa vifungo na uanze kupasi upinde wa kufungia vifungo na kisha upande mzima. Fanya hivyo kwa upande wa vifungo pia ikiwemo kupasi katikati ya vifungo pia.
Na mwisho kabisa ni mikono abayo utainyoosha vizuri na kupiga pasi upade wa mbele na kisha kuugeuza nyuma, fanya hivyo kwa mkono wa pili pia.
Kwa nguo zinazoteleza inashauriwa kuzifunika na kitambaa cha pamba kabla ya kuzipasi ili zisiungue na kutokana na aina ya kitambaa chake.