Kampuni ya usafiri ya Mofat imetangaza nafasi 360 za ajira, zikiwemo nafasi 200 za madereva wa Mabasi Yaendayo Kasi (BRT) na nafasi 160 za Maafisa wa Huduma kwa Abiria.
Kwa nafasi za udereva, waombaji wanatakiwa kuwa na elimu ya msingi, kidato cha nne au kidato cha sita, pamoja na leseni ya udereva Daraja C “Plain” iliyothibitishwa na Jeshi la Polisi. Aidha, wanapaswa kuwa na cheti cha PSV kutoka VETA au NIT, cheti cha BRT kutoka NIT, na uzoefu wa angalau miaka mitatu katika udereva wa mabasi au magari ya abiria.
Kwa upande wa Maafisa wa Huduma kwa Abiria, waombaji wanatakiwa kuwa na cheti, stashahada au shahada ya kwanza katika fani husika kutoka taasisi inayotambulika. Fani zinazokubalika ni pamoja na huduma kwa wateja, usafirishaji na usimamizi wa ugavi (Transport and Logistics), utawala wa biashara, uhusiano wa umma na fani nyingine zinazohusiana.
Kampuni hiyo imeeleza kuwa tarehe ya mwisho ya kupokea maombi kwa nafasi za udereva ni Oktoba 9, 2026, na kwa maafisa wa huduma kwa abiria ni Oktoba 5, mwaka huu.


