Zaidi ya wakazi 130 wa Chandavai, Kaunti ya Lamu nchini Kenya, wamefikisha suala lao mahakamani wakipinga ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha mfanyabiashara Aliko Dangote.
Wakazi hao wanasema mradi huo wenye thamani ya shilingi trilioni mbili za Kenya, sawa na takriban TZS trilioni 40, unaweza kuwaondoa katika maeneo ambayo familia zao zimeishi na kufanya shughuli za kilimo kwa vizazi kadhaa. Wanadai kuwa hawajaandaliwa mpango wa kuwahamisha wala kupewa fidia.
Kesi hiyo imefunguliwa dhidi ya Ofisi ya Rais, Waziri wa Ulinzi, Idara ya Ardhi na Mipango Miji, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC), Mamlaka ya Maendeleo ya Ukanda wa Lamu-Port South Sudan-Ethiopia (LAPSSET), Serikali ya Kaunti ya Lamu, Dangote Industries pamoja na kampuni mbili zinazotajwa kuwa wakandarasi wa mradi huo.
Kupitia nyaraka za mahakama, wakazi hao wameiomba mahakama kuzuia kuendelea kwa ujenzi na uchimbaji wa eneo hilo, wakisema hatua hiyo inaweza kuharibu zaidi mazao, miti, nyumba na mali nyingine, huku ikibadilisha kabisa hali ya ardhi inayobishaniwa.
Wamesema kuendelea kwa shughuli hizo kutafanya mgogoro wa umiliki na matumizi ya ardhi hiyo kuwa mgumu zaidi kutatuliwa.


